November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wapinga hoja zinazotolewa kuhusu demokrasia

Na Bakari Lulela,TimesMajira Online.

TAASISI ya Watetezi wa Rasilimali Wasio na Mipaka (WARAMI), imepinga hoja zinazotolewa na baadhi ya watu hususun kutoka nje ya nchi kwamba Tanzania imerudi nyuma kidemokrasia baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28 mwaka huu kutokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupata ushindi mkubwa.

Akipinga hoja hizo mbela ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Mwenyekiti wa WARAMI, Habibu Mchange amesema madai hayo hayana mantiki yoyote kwani mfumo wa vyama vingi nchini, uko kikatiba na hauwezi kuondoshwa kwa matokeo ya uchaguzi bali kwa mabadiliko ya katiba.

Mchange amesema mfumo wa vyama vingi, haumaanishi uwepo wa vyama vya upinzani bungeni pekee, bali pia uwakilishi katika vyombo vingine vya uwakilishi na maamuzi kama Mabaraza ya Madiwani na Mabaraza ya Serikali za Mitaa.

Amesema uwepo wa vyama bungeni na matokeo ya maamuzi wa wananchi kupitia sanduku la kura na si zawadi au stahili.

Mchange amesema taasisi yake inaamini kuwa demokrasia na mfumo wa vyama vingi, si chanda na pete hivyo si lazima viende pamoja ingawa nyakati nyingine, huenda pamoja.

Mwenyekiti huyo amesema, zipo nchi za chama kimoja zenye demokrasia imara ndani ya chama kimoja mfano China na Vietnam.

Amesema Bunge na Uwakilishi bungeni ni sehemu ya dhana pana ya demokrasia katika kujumuisha ushiriki wa moja kwa moja wa wananchi kwenye mchakato wa maendeleo ya nchi kupitia asasi na jumuiya za kiraia, hiyo inatokana na ukweli kwamba si wakati wote Wabunge hubeba maslahi ya wananchi.

Hata hivyo amesema, ziko nyakati Wabunge husimamia maslahi ya vyama vyao ambayo yanaweza kukinzana na maslahi ya wananchi katika chaguzi, hakuifanyi nchi kutokuwa ya kidemokrasia kwa kuwa demokrasia ni ushiriki wa wananchi katika maamuzi ya hatma ya maisha yao.

Amesema Bunge na Wabunge ni daraja moja kati ya madaraja mengi, yanayowezesha ushiriki wa wananchi pia ubora wa maamuzi, ndiyo kitu muhimu katika uendeshaji nchi na ndiyo mchango muhimu wa demokrasia, ambapo mawazo ya aina tofauti huwezesha kushindanishwa.

Mchange amesema jambo ambalo wachambuzi wengi hawajalitazama, ama wanalikwepa kwa sababu wanazozijua wao ni katika chaguzi zilizofanyika kwenye nchi nyingi mwaka huu, ambapo dunia inakabiliana na janga la COVID 19, mbali na kigezo cha utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa wananchi, kigezo kingine kilichochangia ushindi au anguko la vyama vingi tawala ni namna walivyoshughulikia janga la ugonjwa huo.

“Haishangazi na haiwezi kuwa ni jambo la kustaajabisha kuona wapiga kura wa Tanzania, mbali na mambo mengine yaliyofanywa na CCM, kigezo cha udhibiti wa COVID 19 kimechangia kwa kiasi kikubwa kujenga imani kwa Serikali ya CCM kuongoza,” amesema.