October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Msemaji wa Serikali aridhishwa na utulivu

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Oline,Dodoma

MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Dkt.Hassan Abbasi,ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo,amekamilisha haki yake ya kikatiba kwa kupiga kura katika eneo la Kilimani, jijini Dodoma, huku akipongeza hali ya amani na utulivu.

Katika eneo hilo ambapo pia awali na baadaye walionekana viongozi wengine mbalimbali wa Serikali, chama na taasisi binafsi, Dkt.Abbasi alikaa kwenye foleni kama kawaida na wananchi wengine na alipomaliza kupiga kura akasisitiza:

“Nimekamilisha haki yangu ya kikatiba kwa furaha sana kwa sababu tukiwa pale kwenye foleni tunapiga stori za hapa na pale wananchi walikuwa wanasema sio wote tuliopiga nao kura mwaka 2015, leo wamepata bahati tena kama hii kwa maana ya uhai kushiriki nasi.

Hivyo ni jambo si tu la kikatiba, lakini lenye hisia kubwa kibinadamu na kiroho mtu anapolitimiza.”

Dkt.Abbasi ameeleza kuridhishwa na hali ya utulivu kituoni hapo na kusisitiza kwamba wale ambao hawajakamilisha haki yao wajitokeze kuwahi kabla ya muda uliowekwa na NEC.

“Kituoni kwetu hapa na kwingine nilikopita hapa Dodoma hali ni shwari. Tume imejipanga hasa utaratibu ni mzuri na wa uhakika kwani kila hatua unaelekezwa wasimamizi na makarani wa uchaguzi na mawakala wa vyama wanajiridhisha kwa kila jina linalotajwa.

“Ukiacha kelele za baadhi ya wanasiasa wachache Watanzania wengi wameitikia wito wa amani na wengi tuliopiga nao kura hapa kila mmoja anasema anarejea nyumbani au kwenye shughuli zake kwa ajili ya kuendelea na masuala mengine atasubiri matokeo kuanzia jioni,” amesema Dkt. Abbasi.

Dkt.Abbasi ametumia muda huo pia kuvipongeza vyombo vya habari kwa kazi kubwa waliyoifanya kuripoti kampeni za vyama mbalimbali na kuvitaka kumaliza vyema zoezi hili la uchaguzi kwa kufuata taratibu za Tume hasa katika kutangaza matokeo ya awali hadi yale ya mwisho.