Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online, Mbeya
HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbeya imeweka mkakati wa kununua mtambo maalumu kwa ajili ya kufanya matengenezo na ukarabati wa barabara zilizoharibika, kufuatia changamoto ya ubovu wa miundombinu hiyo inayokadiriwa kuathiri takribani asilimia 80 ya mtandao wa barabara katika halmashauri hiyo.
Mkakati huo unalenga kuboresha hali ya barabara kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), ili kurahisisha usafirishaji wa mazao na shughuli nyingine za kiuchumi, hususan maeneo ya vijijini.
Akizungumza wakati wa kufunga kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Novemba 26, 2026, katika ukumbi wa Halmashauri hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya na Diwani wa Kata ya Usongwe, Aida Haule, amesema ubovu wa barabara ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazowakabili wananchi.
Amesema sehemu kubwa ya wakazi wa halmashauri hiyo hutegemea barabara kusafirisha mazao ya kilimo kutoka maeneo ya uzalishaji kwenda sokoni, hivyo hali ya miundombinu hiyo kuharibika imekuwa kikwazo katika shughuli zao za kiuchumi.
“Ukiangalia mtandao wa barabara zetu, takribani asilimia 80 ni mbovu. Sisi kama Baraza kwa kushirikiana na uongozi wa Halmashauri tumeweka mkakati wa kununua mtambo utakaotumika kufanya marekebisho ya barabara zetu kwa kushirikiana na TARURA na TANROADS.
“Tunataka kuwatoa hofu wananchi kuwa tunachukua hatua za kukabiliana na changamoto ya miundombinu ya barabara katika Wilaya ya Mbeya,” amesema Haule.
Ameongeza kuwa katika kipindi walichopewa dhamana ya kuwatumikia wananchi, watahakikisha wanaweka juhudi katika kuboresha miundombinu hiyo ili maeneo yote yaweze kupitika na wananchi kuendelea na shughuli zao za uzalishaji bila vikwazo.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Iyunga Mapinduzi, Andrea Mwangoni, amesema wakazi wa kata hiyo wanakabiliwa na changamoto ya ubovu wa barabara, hali inayosababisha ugumu katika usafirishaji wa mazao ya wakulima, hasa wanaoishi maeneo ya pembezoni.
Naye Diwani wa Kata ya Ijombe, Johana Yotam, amesema ubovu wa barabara katika eneo lake ni kero kwa wananchi, akitolea mfano wa eneo la Mto Mwambalizi ambako nguzo zilizowekwa kwa ajili ya miundombinu zimeanguka kutokana na maji.
Amesema hali hiyo inahatarisha usalama wa wananchi na kwamba baadhi ya marekebisho yaliyofanyika hayajaleta matokeo yaliyotarajiwa.
Akijibu hoja za madiwani hao, Meneja wa TARURA Wilaya ya Mbeya, Mhandisi Boniface Kasambo, amesema changamoto za barabara zilizowasilishwa zitafanyiwa kazi kadri fedha zitakavyopatikana.
Amesema ufinyu wa bajeti ni miongoni mwa vikwazo vinavyoathiri utekelezaji wa matengenezo ya barabara, lakini taasisi hiyo itaendelea kutekeleza kazi hizo kulingana na upatikanaji wa fedha.


More Stories
Rais apongeza hatua makubaliano kupunguza vifo mama,mtoto
Bilioni 100 kujenga wodi mama,mtoto Tanzania
EWURA watoa elimu udhibiti huduma nishati na maji