Na Moses Ng’wat, Mbozi
MWANAFUNZI wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Manyala, wilayani Mbozi mkoani Songwe, Vanesa Mgala, ameuawa kwa risasi, huku mwanamke mmoja, Eliza Mwashilindi, na mtoto wake mchanga wakijeruhiwa katika tukio linalodaiwa kuhusisha maofisa wa Maliasili na Hifadhi ya Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi.
Eliza amelazwa katika Hospitali ya Mbozi Mission akipatiwa matibabu pamoja na mtoto wake aliyekuwa amembeba mgongoni wakati wa tukio hilo lililotokea Novemba 24, 2026.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Manyala, Dick Silungwe, amesema watu wanne wanaodaiwa kuwa maofisa wa maliasili walifika kijijini hapo kwa gari wakiwa na bunduki mbili, kabla ya kwenda kupekua nyumba ya mwanakijiji aliyetajwa kwa jina la Magala.
Amesema katika upekuzi huo walikamata mkaa uliokuwa umehifadhiwa ndani ya nyumba hiyo, kiasi cha gunia tatu, na kuupakia kwenye gari.
Hatua hiyo iliwafanya wakazi wa kijiji hicho kukusanyika kwa wingi na kupiga kelele, mazingira yaliyosababisha matumizi ya silaha na madhara yaliyosababisha kifo na majeruhi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Akama Shaaban, akizungumza Novemba 27,2026, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema jeshi hilo limeanzisha uchunguzi.
Amesema marehemu
alijeruhiwa tumboni na mikononi na kwamba alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mbozi Mission.
Aidha, amesema Mwashilindi ambaye anaendelea na matibabu alijeruhiwa mkono wa kushoto na paja la mguu wa kushoto.
Ameongeza kuwa tayari askari 8 wa maliasili na hifadhi ya mazingira wanashikiliwa kwa mahojiano.

More Stories
Rais apongeza hatua makubaliano kupunguza vifo mama,mtoto
Bilioni 100 kujenga wodi mama,mtoto Tanzania
EWURA watoa elimu udhibiti huduma nishati na maji