November 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tantrade kuunganisha Wanawake,Vijana na fursa za Soko la Afrika

Na.Mwandishi Wetu,TimesMajira

MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) inaendelea kuweka msukumo katika kuwaunganisha wanawake na vijana wafanyabiashara na fursa za masoko ya kikanda na kimataifa kupitia ushiriki wake katika maandalizi ya kongamano la nne la Women and Youth African Business Forum (WYABF) 2026, litakalofanyika tarehe 30 Novemba hadi 1 Desemba 2026 katika Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam..

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Wanawake Wajasiriamali Tanzania (TAWEN), Balozi Amina Salum Ali, amesema kongamano hilo ni sehemu ya jitihada za mtandao huo kuwawezesha wanawake na vijana kukuza biashara zao na kutumia fursa zinazopatikana katika masoko ya Afrika.

Ameeleza kuwa kongamano hilo ni toleo la nne tangu lilipoanzishwa mwaka 2023 na mwaka huu litafanyika sambamba na maadhimisho ya miaka mitano ya TAWEN.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TAWEN, Florence Masunga, amesema kongamano la mwaka huu litajikita katika biashara za kidijitali, likiwa na lengo la kuwajengea wanawake na vijana uelewa kuhusu matumizi ya teknolojia katika shughuli za biashara, mifumo ya malipo na utangazaji wa bidhaa na huduma.

Ameeleza kuwa washiriki kutoka nchi 15 za Afrika Mashariki na maeneo mengine ya Afrika wanatarajiwa kushiriki, wakiwemo wataalamu, viongozi wa serikali na wadau wa biashara watakaopata nafasi ya kujadili fursa zinazotokana na Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).

Akieleza ushiriki wa TanTrade, Mkurugenzi wa Ukuzaji Biashara Jonathan Nkwabi amesema mamlaka inashirikiana kitaalamu na TAWEN katika maandalizi na utekelezaji wa kongamano hilo ili kuwawezesha wanawake na vijana kupata fursa za biashara, uwekezaji na masoko mapya.

Ameongeza kuwa kongamano hilo litakuwa na vyumba maalumu vya majadiliano ya biashara na uwekezaji (Deals Rooms), vitakavyowaunganisha wafanyabiashara na wawekezaji kwa ajili ya kujadili fursa, kutafuta washirika na kuanzisha mahusiano yatakayoweza kuzaa matokeo halisi ya kibiashara.

Aidha, baadhi ya wanawake na vijana wafanyabiashara walioshiriki katika matoleo yaliyopita ya kongamano hilo wameeleza namna walivyonufaika na jukwaa hilo kupitia kujenga mahusiano ya kibiashara, kupata maarifa na kufungua milango ya fursa mpya za biashara. Wameeleza matarajio yao kuwa toleo la mwaka huu litaendelea kutoa nafasi zaidi za kukuza biashara zao na kufikia masoko mapya.