November 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwigulu ataka tume za uchaguzi SADC kudhibiti upotoshaji mitandaoni

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Mwingulu Nchemba amezitaka Tume za Uchaguzi katika ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuimarisha matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii katika kusimamia uchaguzi, hususan katika utoaji wa taarifa sahihi kwa umma ili kuepusha upotoshaji unaoweza kuathiri amani na mshikamano wa jamii.

Dkt Nchemba ametoa kauli hiyo, Novemba 23,2026 wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Mkutano mkuu wa siku mbili wa 28 wa Mwaka wa Jukwaa la Tume za Uchaguzi za Nchi Wanachama wa SADC (ECF-SADC), unaendelea jijini Dar es salaam.

Amesema mitandao ya kijamii imekuwa na nafasi kubwa katika mawasiliano na usambazaji wa taarifa, hivyo ni muhimu kwa tume za uchaguzi kuhakikisha majukwaa hayo yanatumika kutoa elimu ya mpiga kura, taarifa za uandikishaji na michakato mbalimbali ya uchaguzi.

“Kutokana na kasi ya usambazaji wa taarifa kupitia mitandao ya kijamii, taarifa zisizo sahihi zinapowafikia wananchi zinaweza kuharibu taswira ya taasisi za uchaguzi, kuathiri uaminifu wa mchakato wa uchaguzi na kusababisha migawanyiko katika jamii”amesema

Aidha amesema vijana wengi kwa sasa hutegemea mitandao ya kijamii kupata habari kuliko vyanzo vingine vya habari, hivyo ni muhimu kwa tume za uchaguzi kujenga mikakati ya kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati.

“Matumizi sahihi ya mitandao yanaweza kuongeza ushiriki wa wananchi katika michakato ya kidemokrasia, ikiwemo kuwafikia wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na makundi mengine maalumu ambayo wakati mwingine hukosa taarifa muhimu kuhusu uchaguzi”amesisitiza

Aidha, amewasihi viongozi wa tume hizo kuendelea kujijengea uwezo katika eneo la Akili Unde (AI), ambalo limekuwa likikua na kubadilika kila siku, ili waweze kukabiliana na changamoto zinazotokana na matumizi yake na kutumia fursa zinazojitokeza kuimarisha mifumo ya uchaguzi.

Akizungumzia umuhimu wa mkutano huo, amesema amefurahishwa kupata nafasi ya kukutana na wenyeviti, wakurugenzi na makamishna wa tume za uchaguzi katika kipindi ambacho nchi nyingi haziko katika uchaguzi, akieleza kuwa muda huo ni muhimu kwa kujenga urafiki, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano.

Alisema amehudhuria mkutano huo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye kutokana na majukumu mengine amemtuma kumwakilisha na kuwasilisha salamu za pongezi na heri kwa washiriki.

Katika mkutano huo kaulimbiu ya mkutano huo, ilihusu usimamizi wa uchaguzi na mitandao ya kijamii pamoja na wajibu wa tume za uchaguzi katika ukanda wa SADC.