November 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Daraja Lubanda ni imara, salama kwa watumiaji: Tanroads

Na Moses Ng’wat, Ileje

WAKALA wa Barabara Tanzania (TANROADS) umesema daraja la muda la Lubanda, lililopo katika Mto Kalembo, Kijiji na Kata ya Ibungu, Wilaya ya Ileje, limejengwa kwa kuzingatia uimara na usalama wa watumiaji, huku ukieleza kuwa linatumika wakati ujenzi wa daraja la kudumu ukiendelea.

Katika taarifa yake kwa umma iliyotolewa Novemba 23, 2026 na TANROADS Makao Makuu imeeleza daraja hilo limejengwa kwenye njia ya mchepuo baada ya daraja la awali kuondolewa kupisha ujenzi wa daraja jipya la kudumu lenye urefu wa mita 30.

Ufafanuzi huo unafuatia taarifa ya wasiwasi iliyotolewa Novemba 21, mwaka huu na Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Kapejama Ndile, aliyesema daraja hilo limeanza kuonyesha dalili za kuharibika kabla ya mvua za msimu huu kuanza.

Ndile alisema baadhi ya makontena yaliyotumika kujenga daraja hilo yameanza kuvunjika kutokana na uzito wa magari yanayopita, huku maji yakipenya chini yake katika eneo lenye udongo dhaifu, hali aliyohofia inaweza kusababisha mmomonyoko wa msingi na kuhatarisha uimara wake.

Alisema daraja hilo ni kiungo muhimu kwa wananchi wa maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Ileje, likiunganisha Kalembo, Malangali, Kafule, Ikinga, Bupigu, Isongole, Itumba na Kilumba, hivyo kuharibika kwake kunaweza kuathiri mawasiliano na shughuli za kiuchumi na kijamii.

Katika taarifa yake, TANROADS Makao Makuu imeeleza kuwa daraja hilo limejengwa kwa gharama nafuu huku likizingatia viwango vya uimara na usalama vinavyotakiwa kwa madaraja ya dharura.

Pia imesema eneo hilo lina daraja jingine la dharura aina ya ‘Drift’ linalosaidiana na daraja la makontena kuhakikisha mawasiliano yanaendelea kuwepo.

Akitoa ufafanuzi zaidi, Novemba 23, 2026 mbele ya waandishi wa habari akiwa eneo la daraja hilo, baada ya kufanya ziara ya kukagua hali yake, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Songwe, Mhandisi Silvan Mroka, amesema daraja hilo limejengwa katika eneo lenye mwamba mgumu unaosaidia kuimarisha msingi na nguzo zake.

Amesema daraja hilo limeweza kuhimili mvua tangu msimu uliopita na kwamba linaendelea kufuatiliwa na kufanyiwa marekebisho pale yanapohitajika ili kuhakikisha linaendelea kutumika kwa usalama.

Ujenzi wa daraja la kudumu la Lubanda ni sehemu ya mradi wa barabara ya Isongole-Ndembo-Isoko yenye urefu wa kilomita 52.4, inayojengwa kwa kiwango cha lami na kampuni ya China Road and Bridge Corporation (CRBC).

TANROADS imesema mkandarasi yupo eneo la mradi akiendelea na kazi za barabara pamoja na maandalizi ya ujenzi wa daraja hilo, ambao utaanza baada ya mvua zinazoendelea kunyesha kupungua.