Na.Mwandishi Wetu,TimesMajira
SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limesema limeahirisha uchaguzi mkuu uliokuwa ufanyike Novemba 25 na 26, 2026 hadi Januari 28 na 29, 2027, kutokana na kasoro zilizobainika katika mchakato wa uchaguzi huo, huku likimsimamisha kazi Naibu Katibu Mkuu wake, Rehema Ludanga, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili.
TUCTA imesema uamuzi huo ulifikiwa na Kamati ya Utendaji katika kikao cha dharura kilichofanyika Novemba 14, 2026, kwa lengo la kurekebisha dosari zilizojitokeza na kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa kuzingatia Katiba na taratibu za shirikisho.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam , Kaimu Katibu Mkuu wa TUCTA, Saidi Wamba amesema miongoni mwa kasoro ni baadhi ya majina ya wagombea kutopitishwa na Kamati ya Utendaji, vyama kuwasilisha majina zaidi ya matatu kwa baadhi ya nafasi, pamoja na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi kuonesha upendeleo wa wazi kwa wagombea.

Amesema kasoro nyingine ni kutoshiriki kikamilifu kwa baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi, kuwepo kwa wagombea ambao hawajakidhi vigezo vya kikatiba, kutokuwepo kwa muda wa kutosha wa rufaa kwa wagombea walioenguliwa na baadhi ya vyama shiriki kutokamilisha chaguzi zao.
Wamba amesema kutokana na hali hiyo, Kamati ya Utendaji iliamua kuvunja Kamati ya Uchaguzi na kuunda nyingine mpya ili kushughulikia kasoro hizo kabla ya uchaguzi mkuu.
Katika hatua nyingine, Wamba amesema TUCTA imeamua kumsimamisha kazi Naibu Katibu Mkuu, Rehema Ludanga, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zinazomkabili, ikiwemo kukaidi maagizo ya Rais wa shirikisho ya kuitisha vikao vya Kamati ya Utendaji na kutohudhuria kikao cha dharura cha kamati hiyo.
Amesema tuhuma nyingine ni kuandika barua ya nafasi ya Kaimu Katibu Mkuu bila kufuata utaratibu wa kimamlaka, pamoja na kubadilisha vyeo vya kiuongozi katika barua rasmi za shirikisho bila ruhusa ya mamlaka husika.
“Uamuzi wa kumsimamisha umefanyika kwa kuzingatia kifungu cha 11.4.4 cha Katiba ya TUCTA, toleo la sita la mwaka 2020, kinachoipa Kamati ya Utendaji mamlaka ya kumsimamisha kwa muda mtumishi au kiongozi na kuwasilisha taarifa kwa Baraza Kuu kwa maamuzi zaidi,” amesema Wamba
Aidha, amesema wamepokea taarifa za kuwepo kwa kundi la watu wanaoendesha vikao vya TUCTA jijini Dodoma licha ya maamuzi ya Kamati ya Utendaji, likidai kuwa vikao hivyo havina uhalali na vinaweza kusababisha mgawanyiko ndani ya shirikisho.
Amesema TUCTA inasisitiza kuwa Rehema Ludanga hana mamlaka ya kushughulikia shughuli za Ofisi ya Katibu Mkuu au kutoa taarifa kwa niaba ya shirikisho wakati akiwa amesimamishwa kazi na uongozi.
“Hata hivyo mkataba wa ajira wa Ludanga kama Naibu Katibu Mkuu ulikuwa wa kipindi cha Novemba 14, 2024 hadi Novemba 14, 2026, hivyo kuongeza muda wa ajira yake kulihitaji idhini ya Kamati ya Utendaji,” amesema
Katika hatua nyingine, Wamba amesema Kamati ya Utendaji imeamua kusogeza mbele mchakato wa marekebisho ya Katiba ya TUCTA hadi baada ya kukamilika kwa uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo.
“Tunawaomba wafanyakazi wote nchini kuwa watulivu, kudumisha mshikamano na kuepuka taarifa zinazoweza kuongeza mgawanyiko ndani ya shirikisho letu,” amesema Wamba

More Stories
Umoti:Huhitaji kumpigia mtu simu kupata mafao ya PSSSF
BBM Festival 2026 ya EXIM kulinda madereva
TANESCO yaomba radhi ukosekanaji wa umeme mbeya na songwe