October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Anwani za makazi na postikodi kurahisisha biashara mtandaoni

Na Faraja Mpina WUUM, Dodoma

KATIBU Mkuu wa Wizara Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Dkt Zainab Chaula amesema kuwa ukamilishaji wa mpango mkakati shirikishi wa kukamilisha mpango wa anwani za makazi na postikodi unaotarajiwa kufikia Halmashauri zote nchini utarahisisha shughuli za
biashara mtandao na huduma za posta mlangoni.

Kwa sasa Wizara hiyo ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) na taasisi zilizo chini ya sekta hiyo zipo katika utekelezaji wa mpango mkakati shirikishi wa kukamilisha mpango unaotarajiwa kufikia Halmashauri zote nchini ifikapo mwaka 2022 ili kuipeleka nchi kwenye uchumi wa kidijitali.

Akizungumza katika ziara ya kukagua uwekeaji wa namba za nyumba katika kata Tatu za Chamwino Ikulu, Ipagala na Hazina, jijini Dodoma Dkt. Chaula amesema kuwa, Wizara yao ipo kwenye utekelezaji wa mkakati wa kuhakikisha kila nyumba inakuwa na anwani ya makazi inayojumuisha jina la barabara, mtaa na namba ya nyumba ili wananchi waweze
kufikiwa katika maeneo wanayoishi kwa urahisi na kukuza biashara mtandao na posta mlangoni kuelekea uchumi wa kidijitali.

Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano wa Wizara hiyo, Mhandisi Clarence
Ichwekeleza amesema, mpango wa anwani za makazi na postikodi unatambulika kimataifa, ukamilishwaji wake utasaidia kuongeza fursa za kibiashara na kujiajiri hasa kwa upande wa biashara mtandao ambapo wananchi wataweza kuagiza bidhaa na kuletewa mpaka mlangoni.

Utekelezaji wa zoezi hilo unahusisha Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, TAMISEMI, Halmashauri na wadau mbalimbali ambapo kazi inayoendelea kwa sasa ni uwekaji wa namba za nyumba katika Halmashauri za jiji la Dodoma chini ya mkandarasi SUMA JKT, ambapo jumla ya nyumba 21,947 zitawekewa namba kati ya nyumba 30,152.

Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Justina Mashiba amesema, ushirikishaji wa Serikali na wananchi katika zoezi la uwekaji vibao vya namba za nyumba ndio unaorahisisha kufanyika kwa zoezi hilo huku UCSAF ikiwa imechangia shilingi milioni 60 kwa ajili ya kata tatu za Chamwino Ikulu, Bahi na Hazina zilizopo jijini Dodoma.

Mpango wa uwekaji wa anwani za makazi na postikodi umetekelezwa katika kata 116 nchini kati ya kata 3956, kwenye Halmashauri 18 kati ya 185 nchini na mwitikio wa zoezi hili kwa wananchi ni mzuri kwa sababu wenye manufaa kwa wananchi na Serikali katika ufikishaji wa
huduma za dharura, biashara na huduma za posta.

Faida nyingine za mpango huu kwa Serikali ni kurahisisha ukusanyaji wa kodi, kuimarisha ulinzi na usalama kwa wananchi na kuhudumia wananchi wakati wa dharura za majanga ya moto na dharura ya wagonjwa.