October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC amaliza mgogoro wa viwanja uliodumu miaka 22

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Bukoba

MKUU wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawiro ametatua mgogoro wa viwanja katika mtaa wa Kyebitembe Kata Nshambya Manispaa ya Bukoba, Mkoani Kagera uiodumu kwa zaidi ya miaka 22 ambao pia ulisababisha kuwepo kwa viashiria vya uvunjifu wa amani.

Akiongea katika mkutano wa hadhara na wananchi wa kata hiyo, Kinawiro amesema kuwa, Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba kupitia kwa viongozi wake waliomaliza muda wao wakiongozwa na mstahiki Meya, walipanga kubomoa nyumba za wananchi 374 pamoja na misingi kwa kosa walilolifanya wao awali ambalo sasa limemalizika baada ya serikali kuingilia kati.

Amesema kuwa, serikali ya awamu ya Tano ni serikali ya wanyonge hivyo haipo tayari kuona wananchi wake wakiteseka na kuhangaika kwa makosa ya wataalamu waliokuwa wanahusika na masuala ya ardhi ambao walikuwa wakiuza kiwanja kimoja kwa zaidi ya watu wawili na kusababisha migogoro.

“Mimi nimeletwa Bukoba na Rais kwa ajili ya kuwahudumia wananchi na sio kuona wananchi wakiteseka, mgogoro huu umedumu kwa miaka 22 na kuna watu wamekuwa wakinufaika na mgogoro huu bila kujali wananchi wanaoumia, kuanzia sasa nafuta ramani ya zamani ili ichorwe ramani mpya ambayo itaendana na hali ya makazi ya sasa na kuanzi sasa pia hakuna kubomoa wala kugusa nyumba yoyote iliyojengwa hata msingi,” Amesema Kinawiro.

Amewataka wale wote waliokuwa wakilalamikia viwanja ambavyo tayari vilishauzwa na waliouziwa na tayari wameshajenga, Halmashauri iwatafutie viwanja vingine ndani ya muda mfupi na wale waliokwisha jenga waachwe waendelee na maisha yao.

Aidha awetaka wananchi kwa kushirikiana na Kamati ya urasimishaji walioichagua wenyewe wafanye mchakato wa haraka wa kuchanga pesa kwaajili ya kupimiwa viwanja vyao kwa wakati na kuwawezesha kupata hati ili kila mmoja awe na umuliki unaotambuliwa kisheria.

Mara baada ya mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamati ya urasimishaji, Fakharudini Nuru amemshukuru kiongozi huyo kwa maamuzi aliyoyafanya na kueleza kuwa migogoro hiyo imekuwa ikiathiri shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa kuwa wananchi walikuwa wakiishi kwa marumbano.

Fakharu ameongeza kuwa, ataendelea kuwahamasisha wananchi wenzake ili waweze kuchanga fedha zitakazo wawezesha kupimiwa viwanja vyao na hatimaye kupata hati miliki na kuweza kuondokana na migogoro isiyo ya lazima.

Kwa upande wake, Kaimu Kamishina wa Ardhi Mkoa wa Kagera, Erick Makundi amesema kuwa, baada ya serikali kufutilia mbali ramani ya zamani na hati zote zilizokuwepo, amewataka wananchi hao kufuata utaratibu kabla hawajanunua viwanja wala kuanza ujenzi, na kuongeza kuwa endapowatawahi kuchanga pesa za ulasimishaji basi watapewa kipaumbele cha kupimiwa na suala la kupewa hati miliki halitazidi wiki mbili.

Ikumbukwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli mnamo tarehe 16 mwezi septemba akiwa katika mkutano wa kampeini mjini Bukoba aliagiza serikali ya wilaya Bukoba kuhakikisha wanamaliza mgogoro wa viwanja Kyebitembe mapema mwaka huu ili kuwawzesha wananchi kuishi kwa uhuru na usalama.