Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online,Mwanza
UFUGAJI wa samaki kwa njia ya vizimba umeanza kuwanufaisha vijana kiuchumi jijini Mwanza, baada ya miezi saba ya uwekezaji kuzaa matunda kupitia uvunaji unaotarajiwa kuwaongezea kipato na kuwafungulia fursa za kujiajiri na kuajiri wengine.
Mafanikio hayo yamechochea Serikali kupanga hatua nyingine ya kuwawezesha vijana kuanzisha viwanda vidogo vya kuchakata samaki ili kuongeza thamani ya bidhaa na kukuza biashara zao.

Akizungumza Novemba 18,2026 katika uzinduzi wa uvunaji wa samaki kwenye vizimba chini ya programu ya BBT-Uvuvi Kampasi ya FETA Nyegezi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais–Maendeleo ya Vijana, Dkt.Joel Nanauka amesema,hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuwafanya vijana kuwa wamiliki wa shughuli za uzalishaji badala ya kutegemea ajira pekee.
Amesema Serikali ilitenga sh.bilioni 200 kwa ajili ya uwezeshaji wa vijana, ambapo asilimia 62 ya fedha hizo zinaelekezwa kwenye sekta za uzalishaji, ikiwemo ufugaji.Katika programu hiyo, vijana wamepatiwa mafunzo ya miezi mitatu, mikopo isiyo na riba wala dhamana, vifaa na usimamizi wa kitaalamu.
Dkt.Nanauka amesema,baada ya miezi saba ya uzalishaji, kila mnufaika anatarajiwa kupata faida ya takribani sh. milioni 9, sawa na sh milioni 1 kwa mwezi. Katika uvunaji huo wa vizimba vitatu, samaki walitarajiwa kuuzwa kwa zaidi ya sh.milioni 76.5, huku uvunaji ukifanyika kwa awamu ili kuzingatia mahitaji ya soko.
Pia amesema,marejesho ya mikopo yatafanyika kwa awamu, huku Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ikitarajiwa kuwawezesha vijana kupata asilimia 85 ya uwekezaji unaofuata huku akisitiza kuwa ni muhimu sekta binafsi kushiriki katika kukuza uchumi na kutengeneza ajira kwa vijana ambapo Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 inalenga sekta binafsi kuchangia asilimia 70 ya uchumi wa nchi ikiwemo katika uzalishaji wa ajira.
Kwa upande wake, Meneja wa Kampasi ya FETA Nyegezi na Msimamizi wa Programu ya BBT-Uvuvi Kanda ya Ziwa amesema,mahitaji ya nchi ya samaki kwa sasa ni takribani bilioni 1.2 huku uzalishaji hata ile nusu bado unasuasua. “Kwa hiyo tunapowekeza sasa kwenye vizimba huku ni njia mbadala ya kuhakikisha kwamba tunapata samaki watakotoshaleza nchi,”.
Hata hivyo amesema,bilioni 9.9 zimetengwa kwa ajili ya uwekezaji wa ufugaji wa samaki katika kanda hiyo, zitakazonufaisha vijana 252. Kati ya fedha hizo, Mwanza imetengewa sh. bilioni 1.98 kwa ajili ya vijana 80.
Amesema, vijana wengine 47 wapo Kagera, 40 Musoma na 85 wanatarajiwa kunufaika Chato mkoani Geita huku vizimba vya Mwanza vina uwezo wa kuzalisha tani 240 za samaki na uzalishaji wa Kanda ya Ziwa ukitarajiwa kufikia tani 756 kwa msimu huo mmoja.
Pia amesema,uvunaji wa siku FETA Nyegezi ulihusisha vizimba vitatu vilivyotarajiwa kutoa tani tisa za samaki, kila kizimba kina uwezo wa kuvuna wastani wa tani 3,hivyo mradi huo unasaidia kupunguza uvuvi haramu katika maeneo yaliyokuwa yakitumika kama mazalia ya samaki.
Hata hivyi amesema,hamasa ya vijana kujiunga na programu za ukuzaji viumbe kwenye maji imeongezeka, ambapo idadi ya wanafunzi katika programu hizo imefikia 71 kutoka 30 hadi 41 katika vipindi vilivyopita.

Naye Meneja Miradi wa TADB, Eveline Shayo amesema,benki hiyo imeanza kutoa mikopo kwa vijana kupitia vituo mbalimbali, ambapo jumla ya sh bilioni 4.3 zimefika kwa wanufaika katika vituo vya Nyegezi Mwanza,Alex Aid mkoani Mara na Kemondo mkoani Kagera.Kwa upande wa ziwa mikopo inakaribia sh.bilioni 2 imetolewa, huku vizimba vitatu vilivyovunwa vikiwa na thamani ya sh.milioni 516.
Amesema, TADB itaendelea kusimamia miradi hiyo na kuwataka vijana kurejesha mikopo kwa wakati ili kuwawezesha wengine kunufaika. Pia ameishukuru Serikali kupitia Wizara za Maendeleo ya Vijana na Mifugo na Uvuvi kwa kuwezesha utekelezaji wa miradi inayolenga kuongeza uzalishaji, kipato na ajira kwa vijana.
Mmoja wa wanufaika wa BBT kituo cha FETA Nyegezi Samuel Manyasi amesema,wanatamani kutengeneza fursa kwa vijana wengine walioko mtaani kupitia mradi huo na kuwafanya waonekane wathamani kwenye jamii
“Kimsingi kabla sijaingia kwenye BBT hali ya uchumi ilikuwa ni ngumu, lakini kwa sasa tunashukuru kwa sababu tuna uwezo wa kusaidia pia familia zetu kiuchumi na jamii inayotuzunguka,”.
Naye mmoja wa wafanyabiashara wa samaki Pendo Makala amesema,samaki hizo zinawasaidia kuendelea na biashara hata pindi samaki wa asili wanapokuwa hawapatikani huku akiiomba Serikali itoke bei ili wajasiriamali na wafugaji wote wapate faida.

More Stories
Magereza,VETA kushirikiana kurasimisha ujuzi kwa wafungwa
Serikali kuchunguza ajali ya Mv.Mwanza
GBT yaikaribisha BetSasa sokoni, yaitaka kuzingatia maadili