Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online,Mwanza
SERIKALI imesema itafanya uchunguzi wa kubaini chanzo cha Meli ya Mv.Mwanza kugonga miamba(mawe), ndani ya Ziwa Victoria pamoja na madhara ambayo yameweza kutokea.
Meli hiyo ilipata ajali hiyo majira ya saa 4 asubuhi, baada ya kugonga miamba ya Bismark Rocky, wakati ikifanya majaribio ya kawaida.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 18,2026 kuhusiana na ajali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, CP.Salum Hamduni amesema,meli hiyo ikiwa katika utaratibu wa kawaida wa majaribio ilikwaruza miamba ndani ya Ziwa Victoria.
“Taarifa ya awali ya tukio la ajali ya Meli MV.Mwanza ya asubuhi kukwaruza mwamba majira ya saa 4 ilikuwa katika utaratibu wa kawaida wa majaribio ya mwisho ya kuanza safari ikiwa katika majaribio hayo ndipo ajali hiyo ikatokea,”amesema CP.Hamduni.
Amesema meli iko salama hata hivyo wameisha fanya mawasiliano na Wizara ya Uchukuzi na Waziri wenye dhamana na maelekezo ya Serikali ni utafanyika uchunguzi wa kina kugundua sababu halisi na madhara ambayo yameweza kujitokeza.
“Ni wahakikishie kama mnavyoona meli imebaki hapa ipo salama,lakini tunataka kujihakikishia usalama zaidi kufanya uchunguzi wa kitaalum,kwa kushirikiana na Wizara na vyombo vya ulinzi na usalama na mamlaka nyingine za Serikali pamoja na wataalamu.Upande wa Serikali upande wa kisekta na Mkoa tutarudi kutoa taarifa ili wananchi waweze kuelewa zaidi,”amesema.
Amesisitiza kuwa meli hiyo licha ya ajali hiyo iko salama ambapo timu ya wataalamu ya kuchunguza chanzo itafanya kazi kwa kasi Serikali ya awamu ya sita kwa siku zisizozidi 14, hivyo aliwasihi wananchi wasipotoshwe na taarifa za mitandao ya kijamii kwani meli ilipata ajali ikiwa chini ya wataalamu wa Wizara wakati wa majaribio hayo na haikuwa na abiria.
” Bahati mbaya ikiwa chini ya wataalamu wetu ndipo ikakwaruza miamba na ninachofahamu TASHICO Iko chini ya Wizara ya Uchukuzi, hivyo wataalamu wanaohusika na kutoa ushauri wa masuala ya meli kutembelea ofisi zao ni jambo la kawaida,”ameeleza CP. Hamduni.


More Stories
Magereza,VETA kushirikiana kurasimisha ujuzi kwa wafungwa
Ufugaji samaki wachochea Serikali kupanga kuwawezesha viwanda vidogo
GBT yaikaribisha BetSasa sokoni, yaitaka kuzingatia maadili