Na Fresha Kinasa,TimesMajiraOnline, Mara.
WANANCHI wa Kata ya Nyangoto, Wilaya ya Tarime mkoani Mara, sasa wanauhakika wa kupata huduma za afya wakati wowote, baada ya watumishi wa afya wa Kituo cha Afya cha Nyangoto, waliokuwa wakiishi mbali kujengewa nyumba bora za kuishi katika kituo hicho.
Nyumba hizo tatu, zilizojengwa kwa sh. milioni 335 na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara kupitia fedha za Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii CSR,ambapo nyumba hizo zina uwezo wa kuhudumia familia tano za watumishi.
Nyumba hizo zimeondoa kero ya muda mrefu ya wagonjwa kukosa huduma kwa haraka kutokana na umbali waliokuwa wakiishi watumishi hao nje ya eneo hilo la Kituo cha Afya.
Wananchi hao wameyasema hayo wakati wakizungumza na waandishi wa habari katika kituo hicho ambapo wameshukuru hatua hiyo ya mgodi katika kuimarisha ubora wa huduma.
Wamesema, kabla ya watumishi kuhamia katika nyumba hizo zilizojengwa kituoni hapo walikuwa wakipata adha kubwa hasa nyakati za usiku kupata huduma za dharura, wakiwemo akina mama wajawazito waliokwenda kujifungua.
Mmoja wa wananchi wa eneo hilo Catherine Enock amesema,Mgodi wa Barrick North Mara umesaidia kuimarisha huduma wakati wote, iwe mchana ama usiku wanahudumiwa.
“Kwa sasa tunapata huduma za afya wakati wote, iwe huduma za kawaida ama za dharura,zamani watumishi wa kituo hiki walikuwa wamepanga nje. Tulipokuja kupata huduma kama ni usiku, tulikuwa tunakaa muda mrefu sana tukiwsubiri waje. ,” amesema Enock.
Gabriel Nyankomu, mkazi wa kata hiyo, ameushukuru Mgodi wa Barrick North Mara kwa hatua hiyo kwani imeimarisha huduma kwa wananchi na kuwapa watumishi wa kituo hicho ari na morali ya utoaji huduma, wakiishi katika mazingira mazuri na kuongeza ufanisi wao wa kazi.
“Huduma kwa sasa zipo bora,wagonjwa tunakuja usiku tunapata huduma, sio kama zamani. Jambo hili kwetu wananchi tunafurahia sana na kuona mchango wa mgodi katika maendeleo ya sekta ya afya. Hii ni alama ya kudumu kwetu wananchi ambao tutaendelea kuhudumiwa hapa,” amesema Nyankomu.
Kwa upande wake, Muuguzi Mfawidhi wa Kituo hicho cha Afya, Abduladhimu Ally amesema,ujenzi wa nyumba hizo ulianza Septemba 2025 na kukamilika Machi 2026 kwa gharama ya sh.milioni 335.
Amesema kabla ya nyumba hizo kukamilika, watumishi waliishi nje na kusababisha huduma za dharura kuchukua muda wa nusu saa hadi lisaa limoja ndipo mgonjwa apate huduma lakini kwa sasa ni dakika tano hadi 10 tu mgonjwa wa dharura anahudumiwa, jambo ambalo limeleta mageuzi chanya katika utoaji huduma.
Pia amesema, wanawake wanaojifungua wameongezeka kutoka 250 hadi 300 kwa mwezi, wagonjwa wa nje wakiongezeka kutoka 780 awali hadi 1,000 kwa mwezi, na wagonjwa wanaolazwa wakiongezeka kutoka 266 awali hadi zaidi ya 300 kwa sasa.
“Nyumba hizi tatu
,kati ya hizo Mbili ni ‘two in one’ na moja inajitegemea tunaushukuru sana Mgodi kwa uwajibikaji huu mkubwa unaodumu katika sekta ya Afya na kuchangia ufanisi wa huduma kwa wananchi tunaowahudumia.”amesema Ally.

More Stories
Wanafunzi UDOM wapewa elimu kuzuia ukatili
Uhalifu watisha Mwalo wa Mswahili, polisi waingilia kati
Rhino Rangers yapewa nguvu ya kupanda Ligi Kuu