Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Mwanza
WANANCHI wanaotegemea Mwalo wa Mswahili jijini Mwanza katika shughuli mbalimbali za kiuchumi wamekuwa wakikumbwa na tishio la vitendo vya ujambazi, uporaji wa mali pamoja na wizi wa injini za boti wawapo ziwani,hali inayotishia usalama wao na shughuli zao za kujipatia kipato.
Mwalo huo hutembelewa na zaidi ya watu 800 kila siku kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi, huku takribani wavuvi 300 wakitegemea Ziwa Victoria kwa ajili ya kujipatia kipato na kuendesha maisha yao.

Hayo yamelezwa wakati Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP.Wilbord Mutafungwa akizungumza na wananchi wa eneo hilo katika muendelezo wa kampeni ya Ongea na Kamanda,ambapo wananchi wa Mwalo wa Mswahili wameliomba Jeshi la Polisi kuongeza doria za mtaani ili kudhibiti makundi ya vijana wanaofika eneo hilo kupora simu.
Pia wameomba kuwekwa taa za kuongozea magari na vizuizi vya kupunguza mwendo wa magari katika barabara ya eneo hilo ili kuzuia ajali zinazowakumba watembea kwa miguu, hususani wanawake.
Mmoja wa wavuvi katika mwalo huo Martine Tila amesema,vitendo vya uvamizi vimeshamiri ziwani hadi wakienda kuvua wanaenda wakiwa tumbo joto.
“Wale watu wanapofika pale kitu cha kwanza wanachukia mawasiliano yako ndiyo wanaanza kufanya kazi yao,”amrsema Tila.
Penina Elias amesema,amekumbana na changamoto ya kuibiwa simu za mkopo katika biashara yake, huku akieleza vikwazo alivyokutana navyo wakati wa kufuatilia kesi hiyo mahakamani.
“Ile sehemu waliokuwa wakivutuia bangi wakanyanyuka,nilikuwa naongea na simu nyingine nilikuwa nimeiweka kwenye ziwa,wakanipiga mtama wakabeba simu zangu zote mbili za mkopo ambao nimeisha maliza,”amesema Elias na kuongeza:
“Lakini nikawa nimepeleka kesi Nyegezi wakakamatwa baadae mahakamani wakawa hawafiki,wakapewa adhabu ya kwenda jela miezi sita kwa kuidharau Mahakama.Wamefika mahakamani yule shahidi aliyekuwa ananisaidia wazazi wakamwita wanakumbatia vile vitendo vya watoto wao,wakamwita pembeni wakasema naye akapiga kona,”.
Akizungumza na wananchi hao DCP. Mutafungwa amesema, suala la ulinzi na usalama ni jukumu la pamoja kati ya polisi na wananchi.
Amesema Jeshi la Polisi linaendelea kufanya doria katika maeneo mbalimbali ya ziwa, lakini linahitaji taarifa za mapema kutoka kwa wavuvi pindi wanapoona watu au makundi hatarishi ya usalama wao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi cha Polisi Wanamaji Mkoa wa Mwanza, SP. Wenceslaus Muchunguzi,amewataka wavuvi kuzingatia sheria za uvuvi na mipaka ya nchi ili kuepuka kukamatwa wanapovuka kwenda nchi jirani.
Aidha, amewataka wamiliki wa mitumbwi kuhakikisha vyombo vyao vimesajiliwa, vina namba za utambulisho na vifaa vya usalama yakiwemo maboya yanayolingana na idadi ya watu wanaoingia ziwani.
Naye Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana (OCD), Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Virginia Sodoka,amewataka wadau wa mwalo huo kuwa walinzi wa kwanza wa maeneo yao kwa kutoa taarifa za uhalifu mapema.


More Stories
Wanafunzi UDOM wapewa elimu kuzuia ukatili
Rhino Rangers yapewa nguvu ya kupanda Ligi Kuu
Barrick North Mara yazindua Wiki ya Mahusiano.