November 14, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TTCL yafungua milango ya Kidijitali kwa Watanzania

Na.Mwandishi Wetu,TimesMajira

SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL), limejipanga kufungua milango ya kidijitali kwa Watanzania kwa kupanua huduma za mawasiliano zinazowawezesha kupata intaneti yenye kasi na ubor katika maeneo mbalimbali, ili kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia ya habari na mawasiliano.

Katika kutekeleza azma hiyo, shirika hilo limeendelea kupanua huduma za intaneti kwa kutumia teknolojia ya nyuzi za mawasiliano (Fiber), kupitia mifumo ya Fiber to the Home (FTTH), Fiber to the Office (FTTO) na Fiber to the Room (FTTR), inayolenga kusogeza huduma za mawasiliano karibu zaidi na watumiaji.

Meneja wa Mauzo na Usambazaji wa TTCL, Laibu Leonard, ameyasema hayo leo Novemba 13, 2026, wakati akiwasilisha mada kuhusu nafasi ya shirika hilo katika kuwezesha matumizi ya teknolojia na mifumo ya kidijitali kwenye Mkutano Mkuu wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (Dar -PC), uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Amesema huduma ya Fiber to the Home inalenga kuwapatia wananchi intaneti majumbani na kurahisisha matumizi ya mtandao kwa wanafamilia wote na wageni wanaotembelea nyumba, tofauti na vifurushi vya simu ambavyo kila mtu hulazimika kununua kivyake.

Amefafanua kuwa kupitia huduma hiyo, wanafamilia wanaweza kutumia mtandao mmoja kwa wakati mmoja, jambo linalorahisisha upatikanaji wa mawasiliano na kupunguza gharama za kununua vifurushi tofauti kwa kila mwanachama wa familia.

Kuhusu huduma ya Fiber to the Room, amesema inalenga zaidi nyumba zenye ghorofa nyingi ambazo wakati mwingine hukabiliwa na changamoto ya mawimbi ya Wi-Fi kutofika vizuri katika baadhi ya vyumba kutokana na umbali kutoka eneo lilipofungwa kifaa cha awali.

Amesema TTCL huweka vifaa vya ziada ndani ya nyumba ili kusogeza huduma ya Wi-Fi kwenye vyumba ambavyo havipati mawasiliano vizuri, hivyo kuwawezesha wateja kutumia intaneti katika maeneo mbalimbali ya nyumba zao.

Kwa upande wa Fiber to the Office, amesema huduma hiyo inalenga mazingira ya ofisi na inafanana na inayotolewa majumbani, huku vifaa vya ziada vikiweza kufungwa katika majengo yenye ghorofa nyingi ili kuhakikisha mawasiliano yanafika katika maeneo yote yanayohitajika.

Aidha, amesema TTCL imepata tuzo ya kimataifa Oktoba mwaka huu katika Jukwaa la Kimataifa la Broadband (International Broadband Forum), lililofanyika Vienna, Austria, ikiwa ni kampuni pekee iliyotambuliwa kwa utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya Fiber to the Home nchini Tanzania.

Amesema shirika hilo pia lina huduma ya kifurushi cha Tatu Kabambe kinachojumuisha huduma ya fiber, simu ya mezani na huduma nyingine za mawasiliano kwa gharama ya Sh 70,000 kwa mwezi.

Kuhusu upanuzi wa huduma hizo, amesema TTCL inaendelea na maandalizi ya mradi wa awamu ya pili (Phase II), utakaohusisha maeneo mengi zaidi yakiwemo Kenyerezi jijini Dar es Salaam.

Katika hatua nyingine, Leonald alisema TTCL inaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kukabiliana na vitendo vya utapeli vinavyotumia mitandao ya mawasiliano.

Amesema shirika hilo lina mifumo ya kubaini namba zinazotumiwa na matapeli na kuzifungia, huku likiimarisha ulinzi wa mitandao yake kwa kutumia mifumo ya usalama ikiwemo firewalls, inayosaidia kuzuia watu wasiohusika kuingia katika mifumo yake.

Ameongeza kuwa utapeli wa kimtandao ni changamoto inayozikabili nchi mbalimbali duniani kutokana na mbinu zake kubadilika mara kwa mara, hivyo TTCL itaendelea kuimarisha mifumo yake ya ulinzi kwa kushirikiana na mamlaka husika.

Ametaja Morogoro na Sumbawanga kuwa miongoni mwa maeneo yaliyobainika kuwa na changamoto kubwa ya vitendo hivyo ambapo shirika hilo linaendelea kufuatilia na kuchukua hatua za kukabiliana navyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Dar -Pc, Bakari Kimwanga amelishukuru Shirika hilo kwa kufanikisha sehemu ya Mkutano huo.