November 14, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bunge la vijana lahitimishwa, vijana wahimizwa uongozi bora

Na Joyce Kasiki,Dodoma

BUNGE  Maalum la Vijana 2026 limehitimishwa huku vijana wakihimizwa kutumia maarifa na uzoefu walioupata kujenga uwezo wa uongozi, uwajibikaji na kushiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo ya taifa.

Akizungumza leo Nov.13,2026 katika hafla ya kuhitimisha bunge hilo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ng’wasi Kamani, amewataka vijana kuyatumia mafunzo waliyopata katika maisha yao ya kila siku, akibainisha kuwa uzoefu huo ni maandalizi muhimu kwao kushika nafasi mbalimbali za uongozi serikalini hapo baadaye.

Amesema Bunge hilo linaakisi maono ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliyetamani kuona vijana wenye uthubutu wa kuhoji, kuchambua na kutoa hoja zenye tija kwa maslahi ya taifa, badala ya kukubaliana na kila jambo bila kulitafakari. Amewasisitiza pia vijana kuhakikisha wanapata taarifa sahihi kabla ya kutoa maoni ili waweze kuwasilisha hoja zao kwa wakati na katika maeneo yanayostahili.

Kwa upande wake, Mbunge wa Serengeti, Mary Daniel, amesema Bunge hilo limekuwa fursa muhimu ya kujifunza kwa vijana kutoka vyuo mbalimbali vya Tanzania Bara na Zanzibar, kwa kuwajengea uelewa kuhusu masuala ya uongozi na siasa.

Naye Spika wa Bunge Maalum la Vijana, Anna Denis, amesema washiriki wamepata maarifa kuhusu historia ya Bunge, kanuni na taratibu za uendeshaji wake, namna ya kuuliza maswali, kupitisha miswada ya sheria pamoja na majukumu ya kamati za Bunge.


Amesisitiza kuwa vijana hao wamehitimisha mafunzo hayo wakiwa na uelewa kuwa uongozi ni dhamana inayohitaji nidhamu, uwajibikaji na utumishi kwa wananchi.