
Na Israel Mwaisaka, Rukwa
KATIKA jitihada za kuhakikisha Wanafunzi wanapata chakula shuleni Wananchi wa kijiji cha Nkomolo kata ya Nkomolo wilayani Nkasi wamejitokeza kwa umoja wao kwa njia ya nguvu kazi kulima mashamba ya shule ya msingi na sekondari Nkomolo.
Akiuzungumzia mpango huo Mwenyekiti wa Kijiji Cha Nkomolo Agatus Mizengo alidai kuwa uongozi wa Kijiji kwa kushirikiana na kamati za shule waliona umuhimu wa kuishirikisha jamii katika ufumbuzi wa tatizo la chakula shuleni ndipo walipoamua wao wayalime mashamba ya shule yaliyopo ili kile kitakachoatikana kitumike kwa ajilibya chakula shuleni.
Alisema kufuatia hari hiyo Wananchi walihamasika na kujitokeza kulima mashamba hayo ya shule ambapo kwa ujumla wake Kuna hekari 20 zilizolimwa kwa nguvu ya Wananchi na kuwa kwa kasi hiyo iliyopo wanao uhakika mkubwa wa kuzalisha chakula kingi kitakachotumika kwa ajiri ya chakula shuleni.
Alidai kuwa kwa muda mrefu wamekua wakiutumia utaratibu wa wazazi kuchangia chakula shuleni lakini walikuja kubaini utaratibu huo unawakosesha baadhi ya Watoto haki ya kupata chakula baada ya wazazi wao kutokuwa na uwezo wa kuchangia chakula.
Alisema kitendo cha baadhi ya Watoto kupata chakula na wengine kushindwa kupata chakula kimekuwa kikitengeneza matabaka miongoni mwao na katika kuliondoa hilo walionelea umuhimu wa kulima shamba ambapo watapanda mahindi,maharage na mboga za majani na kupunguza michango toka kwa wazazi.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Kijiji cha Nkomolo, Reina Valentine, alisema mpango huo umelenga kuimarisha upatikanaji wa chakula shuleni ili kuweka mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia, huku akieleza kuwa ushirikishwaji wa wazazi na walezi umekuwa sehemu muhimu ya kufanikisha mpango huo.
Alisema kuwa awali walipata ugumu wa utekezaji wa mpango huo kutokana na uelewa mdogo waliokuwa nao wazazi juu ya masuala ya lishe lakini baada ya kuelimishwa na kuona matokeo kwa wenzao walioanza kutekeleza mpango huo ambapo kwa Sasa Kila mzazi anataka mtoto wake apate chakula shuleni.
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Nkomolo, Godfrey Mwenda, alisema shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 700, ambapo wanafunzi 244 tayari wananufaika na mpango wa kupata chakula shuleni kupitia michango ya chakula inayotolewa na wazazi.
Alisema juhudi hizo zinaendelea kuhamasishwa ili kuhakikisha wanafunzi wengi zaidi wanapata chakula wakiwa shuleni na hivyo kuimarisha mazingira ya kujifunzia.

More Stories
Dkt.Mwigulu mgeni rasmi kilele miaka 40 COSTECH
Homera ampongeza Rais Samia kwa ajenda ya nishati safi
ETDCO yakabidhi mradi wa umeme wa 33kV Mtwara