Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KAMPUNI ya Mawasiliano Yas Tanzania, imeahidi kuendelea kushirikiana na Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi visiwani humo wanapata huduma za kibingwa kupitia kambi za afya zinazoratibiwa na taasisi ya ZMBF.
Ahadi hiyo ilitolewa wakati wa ufunguzi wa kambi ya matibabu ya Afya Bora, Maisha Bora kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar huko Kinduni, Wilaya ya Kaskazini B chini ya udhamini wa Kampuni ya Mawasiliano ya Yas Tanzania.
Kupitia kambi zake za afya, taasisi hiyo imefanikiwa kuwafikia zaidi ya watu 30,400 mpaka sasa.
Wakazi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja wanaweza kufanyiwa uchunguzi wa saratani ya matiti na ya shingo ya kizazi katika kambi hiyo, pamoja na kupata huduma za macho, kinywa, masikio, pua na koo. Pia wana fursa ya kuchangia damu kwa hiari.
Akifungua kambi hiyo, Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui amesema kuwaleta wataalamu karibu na wananchi kunapunguza gharama ambazo familia zingetumia kusafiri kutafuta matibabu. Alisema kambi hizo pia zinawapa wananchi fursa ya kujua hali zao za afya na kupata ushauri wa kitaalam kwa wakati.
Mazrui amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuboresha majengo ya kutolea huduma za afya, vifaa tiba na mazingira ya kazi ya watumishi wa afya.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Mngereza Mzee Miraji, amesema uwekezaji wa Serikali katika kipindi cha kwanza cha uongozi wa Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi ulihusisha hospitali kumi za wilaya.
Naye, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora, Rehema Tukai, amesema Afya Bora, Maisha Bora ni kampeni endelevu na akiwahimiza wananchi kutumia huduma za kinga na tiba zinazotolewa kupitia kambi hizo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Yas Zanzibar, Waqid Mohamed Waqid amesema, ni faraja kwa Kampuni ya Mawasiliano ya Yas kushiriki katika masuala ya kijamii nje ya kusogeza huduma za mawasiliano karibu kwa wakazi wa Zanzibar.
“Tutaendelea kushirikiana na Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation ili wananchi wengi zaidi waweze kuonana na madaktari bingwa na kupata msaada wa kitaalam,” amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Galos Casian Nyimbo, amewahimiza wakazi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi ili wafanyiwe uchunguzi na kupata ushauri wa madaktari bingwa.

More Stories
Wadau waaswa kuwafikia wananchi wanaoishi Pembezoni
Asas apokelewa kwa kishindo Songwe
Mahundi ahimiza sheria kuimarisha malezi na maadili nchini