November 5, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Kijaji atembelea banda la Tanzania maonesho ya WTM

Na.Mwandishi Wetu,TimesMajira

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, ametembelea banda la Tanzania katika Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya World Travel Market (WTM) London, Uingereza, na kujionea ushiriki wa makampuni zaidi ya 30 kutoka Tanzania yanayotumia jukwaa hilo kutangaza huduma zao pamoja na vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini.

Akizungumza mara baada ya kutembelea banda hilo, Dkt. Kijaji amesema maonesho hayo ni miongoni mwa fursa muhimu za kuitangaza Tanzania katika soko la utalii la kimataifa, hivyo Wizara imejipanga kutumia kila fursa inayopatikana kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchini ili kufikia lengo la kuvutia watalii milioni nane.

Amesema katika ziara yake ametembelea mabanda ya washiriki mbalimbali kutoka Tanzania na kufanya mazungumzo nao, huku akiwahimiza kutumia ipasavyo fursa ya kushiriki maonesho hayo kuitangaza nchi, vivutio vyake vya utalii na huduma zinazotolewa, ili kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la utalii duniani.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa wadau wa sekta ya utalii kutumia majukwaa ya kimataifa kujenga mahusiano ya kibiashara, kutafuta masoko mapya na kuvutia watalii wengi zaidi kuitembelea Tanzania.

Katika ziara hiyo, Dkt. Kijaji aliambatana na Mwakilishi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii,Joshua Nassari, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Dkt. Thereza Mugobi, pamoja na Mwakilishi wa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza,Patrick Mwakalobo.