November 5, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Tulia awafariji waathirika wa Mafuriko Mbeya

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online, Mbeya

SPIKA Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Uyole, Dkt. Tulia Ackson, ametoa msaada wa kilo 600 za mchele na Sh milioni mbili kwa wananchi walioathirika na mafuriko kata ya Nzovwe yaliyotokea Novemba 3, 2026, jijini Mbeya.

Mafuriko hayo yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha kwa takribani dakika kumi yamesababisha baadhi ya wananchi kukosa makazi na kuathiri maisha yao.

Akikabidhi msaada huo Novemba 4, 2026, kwa niaba ya mbunge huyo, Afisa Habari wa Taasisi ya Tulia Trust, Joshua Mwakanolo, amesema Dkt. Tulia ameguswa na hali iliyowakumba wananchi hao baada ya kupata taarifa za mafuriko na kuamua kutoa msaada huo.

Amesema licha ya Dkt. Tulia kuondoka katika nafasi ya ubunge wa Jimbo la Mbeya, bado anaendelea kuwa na uhusiano na wananchi na kushirikiana nao katika shughuli mbalimbali za kijamii.

“Kabla ya kuwa Mbunge wa Uyole, Dkt. Tulia alikuwa Mbunge wa Mbeya, hivyo undugu bado unaendelea. Ameagiza kuja kuwaona wananchi na kuwapa pole. Atakaporejea atakuja kuwatembelea kwa sababu bado sisi ni familia na tumekuwa tukishirikiana katika mambo mengi yanayogusa jamii,” amesema Mwakanolo.

Aidha, amesema Tulia Trust imekabidhi kilo 600 za mchele pamoja na Sh milioni mbili kwa Ofisi ya Kata ili kurahisisha uratibu na kuhakikisha msaada huo unawafikia wananchi waliolengwa.

Kwa upande wake, Jackson Mwakifubwa, mkazi wa Nzovwe, amemshukuru Dkt. Tulia kwa msaada huo, akisema umeonyesha moyo wa kujali na mshikamano kwa wananchi waliokumbwa na maafa hayo.

Amesema msaada huo ni muhimu katika kuwafariji na kuwasaidia waathirika kukabiliana na changamoto zilizotokana na mafuriko hayo.