October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yazindua kiwanda kingine uchenjuaji dhahabu

Nuru Mwasampeta na Steven Nyamiti, Chunya

IMEELEZWA kwamba, katika kuboresha mazingira na shughuli za wachimbaji wadogo wa madini nchini, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 4.7 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vitatu vya uchenjuaji wa madini ya dhahabu ili kuwasaidia wachimbaji hao kupata mafunzo kwa vitendo katika hatua mbalimbali za upatikanaji wa dhahabu.

Mafunzo hayo yatakayokuwa yakitolewa kwa wachimbaji wadogo ni pamoja na elimu ya utafutaji, uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu ili kuwawezesha kufanya uchimbaji wenye tija  na kusaidia kuinua vipato vyao na kuongeza mchango wa sekta kwenye pato la taifa.
 
Hayo yalielezwa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo wakati wa makabidhiano na uzinduzi wa kiwanda hicho kilichogharimu shilingi bilioni 1.7 mpaka kukamilika kwake.
 
Naibu Waziri Nyongo ametumia fursa hiyo kuishukuru Kampuni ya Tan Discovery Mineral Consultancy kwa kukamilisha ujenzi wa viwanda hivyo na kuvikabidhi vikiwa katika ubora kwa mujibu wa makubaliano.

Nyongo amesema, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limepewa jukumu la kuhakikisha linasimamia na kuhakikisha ujenzi wa viwanda hivyo vitatu unakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa.
 
Kwa sasa STAMICO limeonesha kuwa ni shirika linalojiendesha kwa faida baada ya kuanza kutoa gawio kwa serikali kwa kiasi kisichopungua shilingi bilioni moja mwaka 2019 na bilioni 1.1 mwaka huu 2020.

Pia ameitaka STAMICO kuthamini gharama kubwa iliyotumika katika ujenzi wa miradi hii na kuweza kuisimamia ipasavyo ili kuleta matokeo chanya hususani katika kuwawezesha wachimbaji wadogo kuzalisha kwa tija kwa kutumia vifaa vyenye teknolojia rahisi na bora walivyowekewa na serikali yao na kutoa kipaumbele kwa wakazi wa maeneo jirani na kilipo kituo ili waweze kunufaika na matunda ya kuwepo kwa mradi huu.

Nyongo pia ametoa wito kwa wachimbaji wadogo wa Itumbi na maeneo jirani kukitumia kituo hicho kujifunza na kupata taarifa mbalimbali kuhusiana na shughuli za utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji pamoja na biashara ya madini kwani kituo kimejengwa kwa ajili yao. 

Amesema, muda uliotumika katika ujenzi wa miradi hiyo, ikiwa ni pamoja na Lwamgasa, Katente mkoani Geita na Itumbi uliokabidhiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango, Augustine Ollal amesema, mradi ulianza mwaka 2016 ambapo mwezi Aprili 2020 viwanda viwili vya Katente na Lwamgasa vilikabidhiwa na uzinduzi wa kiwanda cha Itumbi kinakamilisha mradi wa tatu uliokuwa umesalia.
 
Kwa upande wake Mshauri Mwelekezi na Mjenzi wa kiwanda hicho, Rogers Sezigwa ameishukuru Serikali kwa kutambua uwezo wa kampuni yake inalojishughulisha na utafiti na ujenzi wa mitambo inayotumia teknolojia rahisi kwa wachimbaji wadogo na wa kati ili kuweza kutekeleza ujenzi wa mradi huo pamoja na ile ya Lwamgasa na Katente mkoani Geita.  
 
Amesema, wanatumia teknolojia rahisi ili kuwawezesha wachimbaji hao kutumia mitambo hiyo kwa elimu ndogo wanayopewa na wataalamu wake kwa kipindi kifupi.
 
Mkataba waliopewa uliwataka kubuni na kujenga mtambo wa kuchenjua dhahabu, lakini wakaona ni vema kutumia fursa hiyo kwa kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo katika maeneo ilipo mitambo hiyo ili waweze kufahamu namna ya kuendesha mashine hizo pamoja na elimu nyingine zinazohusiana na uchimbaji, utafutaji na uchenjuaji wa dhahabu watakazokuwa wakipewa.
 
Vijana waliohusika katika ujenzi wa kiwanda hicho na vile vya Katente na Lwamgasa wamewawezesha kwa kuwapa mashimo ya kuchimba ili waweze kujipatia kipato kutokana na uchenjuaji watakaokuwa wakiufanya kiwandani hapo.

Pamoja na kuwapa mashimo hayo, Sezigwa amesema wamewatambulisha vijana hao katika ofisi za wilaya na mkoa ili waweze kuwatumia kutekeleza miradi mingine kwani wameonesha uwezo wa kufanya hivyo.

Aidha amesema kuwa, hatua ya juu zaidi waliyoichukua ili kuwawezesha vijana hao kwa kuanzisha kampuni inayoitwa Tanzim itakayokuwa ikijishughulisha na uendeshaji wa mitambo hiyo. 

Mwenyekiti wa Bodi ya Stamico, Meja Jenerali mstaafu Michael Isamuhyo ameishukuru Serikali kwa namna ilivyoelekeza nguvu zake na fedha katika kuwasaidia vijana na kubainisha kuwa katika kipindi hiki vijana wanatazamwa kwa namna ya pekee katika kuharakisha maendeleo ya jamii.

Amesema, walibaini kuwa, wananchi wengi wanaojihusisha na shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu kuwa ni vijana na hivyo kukiri kuwa ukizungumzia wachimbaji wadogo unazungumzia vijana.
 
Pamoja na hayo, mstaafu Michael Isamuhyo amesema, Shirika la Madini la Taifa kuwa ni pamoja na kufanya tafiti katika maeneo mbalimbali na kubaini mashapo yaliyopo na kutenga kwa ajili ya wachimbaji wadogo.

Katika kutekeleza hilo tayari shirika hilo limefanya tafiti 20 na tatu kati ya hizo zipo mkoani Chunya ambapo ni eneo la Itumbuli, Sangambi na Shoga.

Jukumu lingine ni kukuza uelewa wa wachimbaji kwa teknolojia rahisi na isiyokuwa na athari kwa afya na mazingira pamoja na majukumu mengine mengi.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi waandamizi wa Chama na Serikali kutoka Wizara ya Madini, Tume ya Madini, Stamico, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Chunya na wengine wengi.