Na Mwandishi Wetu, Timesmajira,Online, Mbeya
SERIKALI imeendelea kuimarisha ubora wa huduma za afya nchini kupitia maboresho ya miundombinu na mifumo ya utoaji huduma, ambapo mkoani Mbeya tathmini ya ubora wa vituo vya kutolea huduma za afya kwa mfumo wa utoaji nyota (Star Rating Assessment) imeendelea kutekelezwa katika halmashauri zote za mkoa huo.
Zoezi hilo la kimkakati linalenga kupima viwango vya ubora wa huduma zinazotolewa katika vituo vya afya na zahanati, kubaini mapungufu yaliyopo na kuweka mikakati ya kuyafanyia kazi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, salama na zenye viwango vinavyokubalika.

Tathmini hiyo inatekelezwa kwa ushirikiano wa wataalamu kutoka Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais-TAMISEMI pamoja na timu za usimamizi wa huduma za afya ngazi ya mkoa na halmashauri.
Akizungumza kuhusu utekelezaji wa zoezi hilo, kiongozi wa timu ya wataalamu, Dkt Mbwana Martine, amesema tathmini hiyo inahusisha halmashauri zote saba za mkoa wa Mbeya ambazo ni Jiji la Mbeya, Mbeya Vijijini, Rungwe, Busokelo, Kyela, Chunya na Mbarali.
Amesema tathmini hiyo ni muhimu katika kuhakikisha vituo vya kutolea huduma za afya vinaimarishwa na kuendana na mahitaji ya wananchi, hususan katika kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea na maandalizi ya utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Bima ya Afya kwa Wote.
Ameeleza kuwa maboresho ya vituo vya afya ni sehemu muhimu ya kuhakikisha mfumo huo unatekelezwa kwa ufanisi, huku wananchi wakipata huduma zinazokidhi viwango vya ubora bila kukabiliwa na vikwazo vya kifedha.
Awamu ya Pili ya Bima ya Afya kwa Wote ilizinduliwa rasmi Oktoba 22, 2026, mkoani Mtwara na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, ikiwa ni hatua muhimu katika utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za afya.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa tathmini hiyo mkoani Mbeya ni mwendelezo wa jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI katika kuimarisha mfumo wa afya nchini.
Jitihada hizo pia zinaunga mkono malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, inayosisitiza upatikanaji wa huduma bora, salama, za uhakika na zinazozingatia mahitaji ya wananchi wote.
Kupitia mfumo wa Star Rating, Serikali inalenga kuimarisha uwajibikaji, kuboresha mazingira ya utoaji huduma na kuongeza imani ya wananchi kwa vituo vya afya vya umma.


More Stories
PPG yasogeza huduma za chakula,vinywaji Terminal 3
Kivunge ataka madeni yakusanywe kuboresha miundombinu utalii
Hasira za Ndejembi kwa Tanroads Songwe, zaifanya Tunduma kupumua