November 3, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mashirika ya Kijamii yatakiwa kuimarisha uwezeshaji wanawake,kupambana na ukatili

Na Mwandishi wetu,TimesMajira

TAASISI za kijamii zimehimizwa kuongeza juhudi za kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi na kielimu sambamba na kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili ili jamii iache kuvificha badala yake itoe taarifa kwa mamlaka zinazohusika kwa hatua zaidi za kisheria.

Wito huo ulitolewa na Mwanahabari Mkongwe,Idda Mushi, aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya kuzaliwa kwa Shirika la Wanawake Katika Elimu (SWE), yaliyofanywa mjini Morogoro kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro na Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Kanda ya Mashariki.

Idda Mushi, mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 25 katika tasnia ya habari ambaye pia ni Mwenyekiti wa bodi ya Uongozi wa Shirika lisilo la kiserikali linalohusika na malezi ya watoto wenye uhitaji la Kulea Childcare International, Tawi la Tanzania,alisema vitendo vya ukatili wa kijinsia, ukatili dhidi ya watoto na watu wenye ulemavu havipaswi kufichwa kwa sababu ya hofu, aibu au kulinda mahusiano.

Amesema jamii inapaswa kutambua kuwa kupinga ukatili kwani ni jukumu la kila mtu, likiwahusisha majirani, wazazi, viongozi wa mitaa na vijiji, viongozi wa kata pamoja na viongozi wa dini.

”Kunyamazia matukio hayo kunaweza kuongeza madhara kwa waathirika, hivyo amewataka wanaokumbana na vitendo vya ukatili au wanaovishuhudia kutoa taarifa kupitia Dawati la Jinsia na Watoto la Jeshi la Polisi na mifumo mingine ya mamlaka husika.

”Jamii inapaswa kuwa sehemu ya ulinzi wa watoto, wanawake na watu wenye ulemavu kwa kuhakikisha waathirika hawatelekezwi wala kunyimwa nafasi ya kupata msaada,”amesema

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mwakilishi wa Jeshi la Polisi, Sajinitajini,Aziza Itonye, kutoka Dawati la Jinsia na Ulinzi wa Mtoto, Manispaa ya Morogoro, amesema dawati hilo limekuwa likipokea zaidi ya matukio 20 kwa siku yanayohusishwa na vitendo vya ukatili.

Itonye ametaja matukio ya ubakaji na vipigo kuwa miongoni mwa vitendo vinavyoripotiwa, akisema jamii inapaswa kuendelea kuelimishwa kuhusu namna ya kukabiliana na vitendo hivyo.

Amesisitiza umuhimu wa wananchi kuelewa kuwa taarifa za matukio ya ukatili zinapaswa kufikishwa kwenye mamlaka zinazohusika ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

Katika maelezo yake, Idda Mushi pia alihusisha mapambano dhidi ya ukatili na umuhimu wa malezi bora, akisema elimu ya mtoto haipaswi kuishia kwenye masomo ya darasani pekee, bali inapaswa kuambatana na maadili, heshima na uwajibikaji.

Amesema baadhi ya kauli za matusi na vitisho zinazoonekana kwenye mitandao ya kijamii zikifanywa na baadhi ya mabinti wadogo zinapaswa kupokewa kama changamoto kwa wazazi, walezi na jamii kutafakari nafasi yao katika malezi.

Kwa upande wake, Mwanzilishi wa Shirika la Wanawake Katika Elimu,George Lukoa, amesema shirika hilo limekuwa likipambana kusaidia wanawake na wasichana kujikimu kiuchumi sambamba na kuwapatia elimu katika maeneo mbalimbali.

Amesema programu za shirika hilo zinahusisha elimu ya ujasiriamali, ubunifu, stadi za kidijitali, ulinzi wa mtoto, uongozi na utawala bora, na kwamba hadi sasa limefikia zaidi ya wanawake 5,000.

Lukoa amesema SWE ilianza shughuli zake mwaka 2013 ikiwa na dhamira ya kukuza elimu, uwezeshaji wa wanawake na maendeleo ya jamii.