October 28, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

iTrust yazindua mifuko mitatu ya Uwekezaji

Na Mwandishi wetu,TimesMajira

Kampuni ya iTrust Finance Limited imezindua mifuko mitatu mipya ya uwekezaji wa pamoja inayolenga kuwawezesha Watanzania na wawekezaji wengine kupata fursa za kuwekeza katika kampuni mbalimbali zilizoorodheshwa katika masoko ya hisa barani Afrika, kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Mifuko hiyo inayojulikana kama Pan-African Exchange Traded Funds (ETFs) ni iAfrica Financials ETF, unaowekeza katika hisa za kampuni zinazotoa huduma katika sekta ya fedha, hususan benki na taasisi za fedha; iAfrica Mining & Energy ETF, unaowekeza katika kampuni za nishati na madini; pamoja na iAfrica Telco & Tech ETF, unaowekeza katika kampuni za teknolojia ya habari na mawasiliano.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Masoko na Uchunguzi wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na m(CMSA), Exalt Julius, aliyemwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu wa mamlaka hiyo, CPA Nicodemus Mkama, amesema mifuko hiyo imeidhinishwa baada ya mamlaka kujiridhisha kuwa kampuni ya iTrust Finance Limited imetimiza vigezo vya kisheria vinavyohitajika kwa ajili ya kuanzisha na kuendesha mifuko ya uwekezaji wa pamoja.

Amesema uwekezaji huo unafungua wigo mpana kwa Watanzania kupata fursa za kuwekeza katika kampuni zilizoorodheshwa katika masoko ya hisa ya nchi mbalimbali za Afrika, zikiwemo Afrika Kusini, Misri, Nigeria na Kenya.

“Mifuko hii inampa Mtanzania anuwai ya kuweza kuwekeza sehemu mbalimbali katika kampuni ambazo zimeorodheshwa katika masoko ya hisa ya Afrika,”amesema Julius.

Ameongeza kuwa mifuko hiyo imeidhinishwa kwa kuzingatia sheria na kanuni za masoko ya mitaji na dhamana, huku akiwahimiza wananchi kujifunza kuhusu fursa na vihatarishi vya uwekezaji kabla ya kufanya maamuzi ya kuwekeza.

Kwa upande wake,Mkurugenzi wa iTrust Finance Limited, Profesa Mohammed Warsame,amesema uzinduzi wa mifuko hiyo mitatu unalenga kuwapa wawekezaji nafasi ya kupanua uwekezaji wao katika sekta mbalimbali za uchumi wa Afrika badala ya kutegemea soko au sekta moja pekee.

Amesema iAfrica Financials ETF utawekeza katika hisa za kampuni zinazotoa huduma katika sekta ya fedha, hususan benki na taasisi za fedha; iAfrica Mining & Energy ETF utawekeza katika kampuni za nishati na madini; huku iAfrica Telco & Tech ETF ukiwekeza katika kampuni za teknolojia ya habari na mawasiliano.

“Kwa Mtanzania, inamaanisha kwamba sasa anaweza kuwekeza katika mifuko hii mitatu inayowekeza Afrika nzima kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam,”amesema Profesa Warsame.

Ameeleza kuwa kuwekeza katika sekta tofauti kunaweza kusaidia kusambaza vihatarishi vya uwekezaji, kwa kuwa mwenendo wa sekta moja unaweza kutofautiana na mwingine kulingana na hali ya uchumi na masoko.

Naye Meneja wa Mifuko wa iTrust Finance Limited, Francis Samkyi, amesema kampuni imeweka lengo la kukusanya shilingi bilioni 10 kwa kila mfuko, huku ikitarajia kupata uwekezaji unaozidi kiwango hicho kutokana na mwitikio wa wawekezaji.

“Hivi ni vyombo vipya vinavyoweza kusaidia jamii ya Tanzania na kila mwekezaji anayetaka kuwekeza barani Afrika,”amesema Samkyi.

Amesema mifuko hiyo itawapa wawekezaji fursa ya kupanua wigo wa uwekezaji wao nje ya nchi wanazoishi, huku akifafanua kuwa kampuni haiwezi kutaja kiwango maalumu cha faida kitakachopatikana kwa kuwa bei za hisa hubadilika kulingana na mwenendo wa soko.

Hata hivyo, amesema kampuni ina matumaini ya kuona mifuko hiyo ikifanya vizuri, akirejea uzoefu wa mfuko wa uwekezaji wa iTrust unaolenga soko la Afrika Mashariki uliozinduliwa Januari mwaka huu.

Kuhusu usalama wa fedha za wawekezaji, Samkyi alisema mifuko hiyo ina Benki ya NBC kama mdhamini na mwangalizi, huku CMSA ikiendelea kutekeleza jukumu lake la kusimamia sekta ya masoko ya mitaji na dhamana kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizowekwa.

Uzinduzi wa mifuko hiyo unalenga kuongeza fursa za ushiriki wa wananchi katika masoko ya mitaji, kupanua wigo wa uwekezaji na kuwawezesha wawekezaji wa ndani kupata fursa katika sekta mbalimbali za uchumi wa Afrika.