Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
BODI ya Utalii Tanzania (TTB) imezindua kampeni ya CODE +255 – TWENZETU KUTALII, inayolenga kuwahamasisha Watanzania kutembelea na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii nchini kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka.
Kampeni hiyo imeanza kutekelezwa leo Oktoba 27, 2026 hadi Januari 15, 2027, itashirikisha watu maarufu, washawishi wa mitandao ya kijamii na Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) kutangaza vivutio hivyo na kuhamasisha utalii wa ndani.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Dkt. Thereza Mugobi, amesema zaidi ya mabasi 400 yanatarajiwa kuwekwa maudhui ya utalii ili kuwafikia abiria wengi na kuwafahamisha vivutio vinavyopatikana katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema kampeni hiyo pia itahusisha ofa na vifurushi maalumu vya safari kwa gharama nafuu, ili kuwawezesha Watanzania wa makundi mbalimbali kushiriki utalii kulingana na uwezo wao.
“Kampeni yetu hauishii kwenye hifadhi za wanyamapori pekee, bali unahusisha pia fukwe, maeneo ya kihistoria, utamaduni, vyakula vya asili, sanaa na matamasha, ambavyo vinaweza kuongeza kipato kwa wajasiriamali na watoa huduma mbalimbali,”

Makamu Mwenyekiti wa TABOA, Mbazi Mbazi, amesema chama hicho kinaunga mkono kampeni hiyo na kitaweka utaratibu wa kuhakikisha mabasi yanatumika kutangaza vivutio vya utalii kupitia filamu na chaneli zinazoonyeshwa kwa abiria.
“Tumejiandaa magari yetu yatatumika kusafirisha abiria kwenda maeneo mbalimbali yenye vivutio vya utalii, huku wananchi wakiangalia filamu. Tunafanya hivyo kwa sababu jambo hili ni la kizalendo na tupo tayari kuitangaza nchi yetu,” amesema Mbazi.
Mtengengeza Maudhui mtandaoni Fadhil Atick, maarufu Mr Pengo, amesema ataandaa maudhui yatakayohamasisha Watanzania kutembelea vivutio vya utalii, huku mwigizaji Leah Mwendamseke, maarufu Lamata, akisema atatumia ushawishi alionao kutangaza utalii na kuwa mfano kwa kutembelea maeneo mbalimbali.

Kwa upande wake, Maxwell Alfred , maarufu Mzee Shayo, amesema Watanzania wanapaswa kutumia fursa ya utalii wa ndani kwa kuwa gharama za kutembelea baadhi ya vivutio ni nafuu ikilinganishwa na viwango vinavyotozwa watalii wa wageni.
Akitolea mfano, amesema kiingilio cha Sh5,900 kwa Mtanzania ni nafuu ikilinganishwa na dola 30 za Marekani, sawa na takribani Sh79,000, kwa mgeni.
Naye Muigizaji, Leah Mwendamseke ( Lamata) amesema kupitia ushawishi walionao wataendelea kutangaza utalii pamoja na wao kuwa mfano kwa kutembelea maeneo mbalimbali.

More Stories
Serikali kupeleka umeme vitongoji vyote Igalula
Wanafunzi Babati watakiwa Kutoa elimu ya uhifadhi na mabadiliko ya tabia Nchi vijijini
Yas yawajengea uwezo wanawake 150 Mwanza