Na Moses Ng’wat, Mlowo
WAMILIKI 165 kati ya 170 wa maeneo yaliyotwaliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Mkoa wa Songwe, wamelipwa fidia kupisha upimaji wa viwanja vya makazi katika Mji wa Mlowo, hatua inayolenga kuupanga mji huo kisasa na kudhibiti makazi holela.
Hoja ya fidia kwa wamiliki hao iliibuliwa katika kikao cha baraza la Mamlaka ya Mji Mlowo kilichofanyika leo, Oktoba 23, 2026, katika Shule ya Sekondari Dkt. Samia, kitongoji cha Lutumbi.
Akitoa ufafanuzi nje ya kikao hicho, Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji Mlowo, Bosco Njate, amesema wamiliki hao 169 waliolipwa fidia ni wale waliokuwa wakimiliki maeneo tao katika vitongoji vya Saganoti, Izila na Tazara.

Amesema mpango huo umetokana na uhitaji wa kupanua na kupanga mji huo, ambao maeneo yake yamebanana, ili kuwezesha upatikanaji wa viwanja vilivyopimwa na kudhibiti ujenzi holela.
Njate amesema kabla ya kuanza kwa zoezi hilo, wananchi walipatiwa elimu kupitia watendaji wa vitongoji na kata kuhusu umuhimu wa mpango huo na kuukubali, kabla ya Idara ya Ardhi kuanza kutambua wamiliki na kufanya taratibu za ulipaji fidia.
Amesema wamiliki ambao hawajalipwa wanapaswa kufika Idara ya Ardhi kurekebisha kasoro hizo ili kukamilishiwa malipo yao.

Ameeleza kuwa baada ya kukamilika kwa zoezi la fidia, Halmashauri itaendelea na hatua za kupima eneo hilo na kuandaa miundombinu muhimu, ikiwamo barabara za mitaa.
Njate amesema hatua hiyo itafungua njia ya kuanza mchakato wa uuzaji wa viwanja, huku upangaji rasmi wa eneo hilo ukitarajiwa kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii kama maji na umeme.
Mpango huo pia unalenga kuongeza thamani ya ardhi na kuimarisha ukuaji wa Mji wa Mlowo kupitia makazi yaliyopangwa na viwanja vilivyopimwa rasmi.
Hivi karibuni akizungumza na vyombo vya habari, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Maarifa Mwashitete, alibainisha kuwa Halmashauri imetenga kiasi cha sh. Mil 600 kwa ajili ya kutwaa ardhi katika maeneo ili kupanga mji wa kisasa.


More Stories
Wajumbe Mamlaka waridhishwa ujenzi wa shule mpya Mlowo.
COPRA yawataka vijana kukimbilia kilimo kutimiza Dira 2050
Mfumo kidijiti kuondoa urasimu bima afya kwa wote