Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online,Tandahimba
MGOMBEA urais wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ameitaka CCM kuacha kusingizia ugonjwa wa Corona kuwa ndiyo uliosababisha bei ya korosho kuporomoka na badala yake Serikali ya CUF itahakikisha inajenga mazingira mazuri ya kufanyia biashara ikiwa ni pamoja na kujenga viwanda vya kubangulia korosho.
Prof. Lipumba ameyasema hayo wakati akiomba kura za urais, ubunge na udiwani kwa wananchi wa Vijiji vya Mahuta, Matogoro, Mihambwe na Nanyamba vilivyopo Jimbo la Tandahimba mkoani Mtwara.
Prof. Lipumba amesema tatizo la Serikali ya CCM haijajenga mazingira mazuri ya biashara na badala yake imekuwa ikisingizia ugonjwa wa Corona, kwamba ndiyo umesababisha kushuka bei ya korosho.
“Mwaka 2019 hapakuwa na ugonjwa wa Corona na bei ilikuwa mbaya, wakulima wengi walikopwa kabisa. Mwaka huu kweli kulikuwa na ugonjwa wa Corona, lakini nchini Vietnam wameudhibiti na korosho haziambukizi maradhi,”amesisitiza.
Ameongeza kuwa korosho zinasafirishwa kwenye meli sio watu, hazina virusi vya Corona kwa hiyo wasidanganye kwamba bei ya korosho imeporomoka kwa sababu ya ugonjwa huo.
Aidha amewaomba wananchi wampe kura ili aweze kujenga viwanda vya kubangua korosho ili wanunuzi wafike kuzichukua na kuzipeleka kwenye maghala yao kwa ajili ya kukuza masoko yao.
“Sera za CCM zisizokamilika zimesababisha viwanda kutojengwa, wenye viwanda wanahitaji korosho zikishakomaa waanze kuzinunua na kuzipeleka kwenye maghala yao wanaambiwa hawana ruhusa ya kuzinunua mpaka zipitie kwenye utatatibu wa stakabadhi, matokeo yake mtu anayetaka kuanzisha kiwanda cha kubangua korosho anajikuta hana uhakika kupata malighafi ya kuweza kuitumia kwenye kiwanda chake,”amesisitiza Prof. Lipumba.
Katika hatua nyingine, Profesa Lipumba alielezea kusikitishwa na hali ya miundombinu ya barabara za kuelekea vijijini Tandahimba tatizo ambalo limekuwepo kwa miaka 50 ya Uhuru.
Amesema ubovu huo wa barabara unachangia kipato cha wananchi kupungua kutokana na kutumia gharama kubwa katika usafiri.
Amezingumzia suala la kuwepo kwa mfumo mzuri wa kodi, Prof. Lipumba amesema Serikali yake itahakikisha biashara mpya zinafunguliwa na wenye viwanda waweze kumudu uendeshaji wa viwanda vyao.
Amesema mazingira ya ulipaji kodi yanatakiwa yaandaliwe vizuri ili mapato ya Serikali yatokanayo na kodi yaweze kuwa makubwa na ya kuridhisha.
“Katika ilani yetu tutaangalia upya viwango vya kodi, Serikali ya umoja wa kitaifa chini ya CUF itavipitia upya viwango vyote vya kodi zinazotozwa na Serikali Kuu kwa nia ya kuvirekebisha visiwe ni kero kwa walipa kodi,”amesema.
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea