Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Mwanza
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamsaka dereva wa basi la kampuni ya Africa Raha lenye namba za usajili T 715 ETS, aina ya Yutong, aliyetoroka baada ya basi alilokuwa akiendesha kugonga treni katika eneo la Fela wilayani Misungwi mkoani Mwanza na kusababisha majeruhi sita.
Akitoa taarifa hiyo kwa umma, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP. Wilbrod Mutafungwa amesema,ajali hiyo imetokea leo majira ya saa 7 mchana katika makutano ya barabara inayotoka Usagara kuelekea Kisesa na njia ya reli.

Amesema basi hilo lilikuwa na abiria 22, likitokea Stendi ya Nyegezi kuelekea mkoani Mara, lilipofika katika makutano hayo dereva alishindwa kusimama na kuchukua tahadhari, hivyo kupita katika njia ya reli na kugongwa katikati na treni aina ya kiberenge iliyokuwa ikitokea mjini kuelekea upande Malya.
Kwa mujibu wa DCP. Mutafungwa, ajali hiyo imesababisha basi kusukumwa na kutupwa pembeni, huku abiria sita wakipata majeraha na kupelekwa katika Kituo cha Afya Kisesa kwa ajili ya matibabu.
Hata hivyo amesema, majeruhi hao wanaendelea kupata matibabu, huku baadhi yao wakiwa wamepata mshtuko mkubwa kutokana na tukio hilo huku mmoja wa majeruhi amekimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou-Toure kwa ajili ya matibabu zaidi.
Vilevile ameeleza kuwa, hali za majeruhi si mbaya, huku jitihada za kumtafuta dereva wa basi hilo zikiendelea baada ya kutoroka eneo la tukio.
Sanjari na hayo ametoa wito kwa madereva wa magari ya abiria na watumiaji wengine wa barabara kuzingatia alama za usalama barabarani, hususani katika maeneo yenye makutano ya barabara na reli.
Amesisitiza kuwa madereva wanapaswa kuchukua tahadhari zaidi katika eneo hilo kutokana na kuendelea kwa shughuli za ujenzi wa mradi wa Reli ya Kisasa (SGR), ambapo alama za tahadhari zimewekwa kuwaelekeza watumiaji wa barabara namna ya kupita kwa usalama.
Pia amewataka kuheshimu alama hizo na kuhakikisha wanakuwa makini wanapokaribia makutano ya reli ili kuepusha ajali zinazoweza kusababisha majeraha, vifo na uharibifu wa mali.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Johari Samizi amewataka madereva na watumiaji wote wa barababara kuwa makini kwa kuangalia alama za barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.
Naye dereva wa Treni hiyo ya mizigo Twarib Hassan Mrope, amesema wakati ajali hiyo inatokea wote walikuwa katika mwendo wa polepole lakini hajui kitugani kilitokea kwa derva wa basi na kusababisha ajali hiyo.


More Stories
Afrika yatathmini mikakati ya kuimarisha usafiri wa majini
Dkt.Mwigulu :Nchi za Afrika imarisheni usafiri wa majini
TRA yapongezwa kwa makusanyo ya kodi