Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Kibaha
ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani, Dkt. Rogers Shemwelekwa, amekabidhi ofisi kwa Mkurugenzi mpya, Warda Maulid, akiwa ameacha rekodi imara ya kifedha cha ikiwa na zaidi ya sh.bilioni 16 benki, hali inayoonesha halmshauri hiyo ina ukwasi mkubwa (uwezo mzuri wa kifedha).
Shemwelekwa amesema tangu alipoingia katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Mjini, makusanyo ya mapato yameongezeka kutoka sh.bilioni 7 mwaka 2024/2025 hadi kufikia sh.bilioni 18, sawa na ongezeko la sh.bilioni 11.

Amesema kwa mwaka wa fedha 2026/2027, kuanzia Julai hadi Septemba 30, halmshauri hiyo tayari imefikia asilimia 50 ya makusanyo, huku akieleza kuwa anaamini Mkurugenzi mpya ataendeleza kasi hiyo na kufikia malengo yaliyowekwa.
Pia amesema, halmshauri hiyo imejiwekea lengo la kukusanya kiasi cha sh.bilioni 30 ifikapo 2030, sambamba na kuanzisha vyanzo vipya vya mapato katika eneo lenye ukubwa wa ekari 26, ambako sh bilioni 1.18 zimetengwa kwa ajili ya maegesho ya magari, kituo cha mafuta na shughuli nyingine za kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Warda Maulid, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini na kuahidi kufanya kazi kwa uadilifu na kushirikiana na watumishi katika kuendeleza maendeleo ya halmshauri hiyo.
Kwa upande wake Mbunge wa Kibaha Mjini, Silvestry Koka amesema,matarajio ni kuwa Warda ataongeza chachu ya maendeleo kwa wananchi, huku akimpongeza Shemwelekwa kwa mchango wake katika kuongeza mapato na kuimarisha halmshauri hiyo.



More Stories
TUWASA yaboresha utoaji huduma
Ndejembi apeleka ujumbe wa Tanzania Afrika
Dkt.Homera:Upatikanaji wa Mafuta nchini ni kipaumbele