Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Tabora
MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tabora (TUWASA) imeanza kuboresha huduma za maji kwa wateja kwa kutekeleza mradi wa ufungaji mita za maji za malipo kabla ambapo kiasi cha shilingi milioni 192.5 kitatumika.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka hiyo Mhandisi Mayunga Kashilimu alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka huu mjini hapa.
Ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboreshwa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi kwa kutumia mita hizo.
Amefafanua kuwa gharama za kununua na kufunga mita 400 za malipo kabla ni kiasi cha sh.milioni 192.5 ambazo ni miongoni mwa sh.milioni 299.1 zilizotolewa na Serikali kupitia Mfuko wa Maji.
“Kiasi hicho kimelenga kutekeleza mradi wa ununuzi wa dira za maji kwa ajili ya mtandao wa maji Sikonge na Tabora Manispaa ili kuboresha usambazaji wa huduma hiyo.Awamu ya kwanza wateja 350 watanufaika na mradi huu katika eneo la Tabora Manispaa na 50 eneo la Sikonge, tutahakikisha zoezi hilo linaendelea kwa wateja wote 41,402 wanaohudumiwa na TUWASA hadi sasa,”.
Pia alimhakikishia Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kuwa TUWASA ina dhamira ya dhati ya kufunga mita hizo kwa wateja wake wote ili kuongeza ufanisi kwenye ukusanyaji mapato na kupunguza malalamiko ya wateja.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Mwang’onda ameeleza kufurahishwa na mradi huo kwa kuwa utapunguza upotevu wa maji kwa kiasi kikubwa na kuongeza mapato ya mamlaka hiyo.
Ameongeza kuwa mradi huo ni muhimu kwa kuwa utasaidia kupunguza malalamiko ya wananchi kubambikiwa bili, hivyo akawataka kuharakisha utekelezaji wake katika Ofisi za Mkuu wa Wilaya na kwa wateja wengine
Mwisho.

More Stories
Warda akabidhiwa rasmi ofisi Kibaha
Ndejembi apeleka ujumbe wa Tanzania Afrika
Dkt.Homera:Upatikanaji wa Mafuta nchini ni kipaumbele