October 2, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nimekuja kuiunganisha timu ya maendeleo si kutawala:Magomi

Na Moses Ng’wat, Mbozi

MKUU mpya wa Wilaya ya Mbozi, Farida Mgomi, amesema kuhamishiwa kwake wilayani humo si kwa ajili ya kutawala, bali kuunganisha nguvu za viongozi, watendaji na wananchi katika kuharakisha maendeleo.

Mgomi ameyasema hayo Oktoba Mosi, 2026, katika hafla fupi ya kukabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Hamad Mbega, ambaye naye kahamishiwa Wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma.

Amesema atashirikiana na viongozi, watendaji na wadau mbalimbali kuhakikisha Mbozi inapiga hatua, akitaja kuongeza mapato ya ndani yanayofikia Sh bilioni 11 kwa sasa kuwa miongoni mwa maeneo atakayoyapa kipaumbele.

“Sijaja kutawala, nimekuja kuunganisha timu ya mapambano ili tulete maendeleo na ustawi kwa wananchi,” amesema Mgomi.

Amesema kuongeza mapato ya ndani ni muhimu katika kuimarisha uwezo wa wilaya kutekeleza miradi ya maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi.

Aidha, amewataka watumishi na watendaji kufanya kazi kwa bidii, kujituma na kushirikiana, huku akisisitiza umuhimu wa kuheshimiana katika utekelezaji wa majukumu.

Kwa upande wake, Mbega, ambaye amehamishiwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumpa nafasi ya kulitumikia Taifa.

Mbega amesema licha ya kuondoka Mbozi, ataendelea kuwa balozi wa kutangaza mema ya wilaya hiyo na kuenzi ushirikiano alioupata wakati wa kulitumikia.

Hafla hiyo pia ilitumika kwa aliyekuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbozi, Mbwana Kambangwa, kuaga baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, mkoani Manyara.

Aidha, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Abdalah Nandondene, naye aliaga baada ya kuhamishiwa Halmashauri ya Newala, mkoani Lindi.