October 1, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

VETA Moshi yaonesha mfumo mpya migodini Geita

Na Joyce Kasiki, Geita

CHUO cha Ufundi Stadi cha VETA Moshi kimeonesha mfumo wa kisasa wa ufundishaji wa Instrumentation and Automation unaotumia upepo na umeme, unaolenga kupunguza gharama za kuajiri wataalamu wa nje migodini nchini.

Mhadhiri wa chuo hicho, Ombeni Tarimo, amesema hayo katika maonesho yanayoendelea Geita, ambapo alisema mfumo huo umebuniwa mahususi kwa ajili ya migodi kwani unasaidia kuendesha mitambo kama vile actuators na valves katika mitambo ya kuchakata madini.

Tarimo amesema kozi hiyo inawajengea wanafunzi uwezo wa kufanya matengenezo, kutambua hitilafu na kubuni saketi mbalimbali zinazotumika migodini, ikiwemo mifumo ya hydraulic na programu za PLC.

Amesema kozi ya Instrumentation and Automation ilianzishwa miaka minne iliyopita kutokana na mabadiliko ya teknolojia katika sekta ya madini na viwanda, na hadi sasa wanafunzi wao wameanza kupata nafasi za mafunzo kwa vitendo katika Mgodi wa Shanta.

“Wadau wengi wanalalamika kukosa mafundi wa ndani,sisi tuna bidhaa tayari. Badala ya kuleta watu kutoka nje kwa gharama kubwa, wanaweza kuwaajiri vijana wetu,” amesema Tarimo.

Kwa upande wake, mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa fani hiyo, Johnny Minde, alisema alichagua kusoma fani hiyo kutokana na kasi ya ukuaji wa teknolojia ya otomatiki migodini na viwandani.

Minde amesema migodi mingi sasa inaendeshwa kwa kompyuta na mifumo ya kujitegemea, hivyo uhitaji wa wataalamu wa mifumo ya kidijitali unaongezeka na fursa za ajira zipo.

“Nawahamasisha vijana wenzangu kuja kusoma fani hii VETA Moshi. Kazi zipo kwa sababu teknolojia inaendelea kukua na migodi inahitaji vijana wenye ujuzi huu,” amesema Minde.

Amesema matarajio yake baada ya kuhitimu ni kufanya kazi katika viwanda na migodi mbalimbali na kusaidia kubadilisha mifumo ya analojia kwenda dijitali.