October 1, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanufaika mikopo ya asilimia 10 Mbozi waaswa

Na Moses Ng’wat, Mbozi

WANUFAIKA wa mikopo ya asilimia 10 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, wameaswa kutumia fedha walizopewa kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuongeza tija katika shughuli zao za kiuchumi na kuboresha maisha.

Nasaha hizo zilitolewa Septemba 30, 2026 na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Maarifa Mwashitete, wakati wa hafla ya kukabidhi mikopo hiyo iliyofanyika Stendi ya Malori mjini Vwawa.

Halmashauri hiyo imetoa mikopo yenye thamani ya Sh milioni 863.5 kwa vikundi 60 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Mwashitete, aliyekuwa mgeni rasmi akimwakilisha aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, aliwataka wanufaika kutumia fedha hizo katika shughuli walizoomba na kuepuka matumizi binafsi yasiyo na tija.

Pia aliwataka kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kuwawezesha wananchi wengine kunufaika na fursa hiyo, akiwataka kuepuka matumizi yasiyo ya msingi, ikiwemo kununua simu za gharama kubwa.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mbozi, Onesmo Mnkondya, aliwataka watendaji wa Halmashauri hiyo kuwasaidia waombaji kukamilisha taarifa na nyaraka zao kwa wakati ili kuondoa ucheleweshaji wa upatikanaji wa mikopo.

Mnkondya alisema baadhi ya vikundi vimekuwa vikirejeshwa kutokana na kutokamilisha nyaraka, hali inayowafanya kupoteza muda na kuchelewa kunufaika na fursa hiyo.

“Unakuta kikundi kinarejeshwa kwa sababu hakijakamilisha katiba ya kikundi tu, halafu wanaanza kupiga simu kwa mbunge au madiwani,” alisema.

Alisema watendaji wanapaswa kukaa pamoja na waombaji na kuwasaidia kutatua changamoto za ukamilishaji wa taarifa, badala ya kuwaacha wakikwama na kutafuta msaada kwa viongozi wa kisiasa.

Naye Katibu wa UVCCM Wilaya ya Mbozi, Haji Mwalim, alisema serikali haipaswi kuwaonea haya wanufaika wanaoshindwa kurejesha mikopo, huku akiwataka watendaji kuepuka kutoa mikopo kwa misingi ya urafiki au upendeleo.

Mwalim pia aliwataka wanufaika wa mikopo ya vyombo vya moto, hususan bajaji na bodaboda, kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani, ikiwemo kuwa na leseni halali.