Na Joyce Kasiki, Geita

OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesisitiza umuhimu wa matumizi ya takwimu rasmi katika kufanya maamuzi na kupanga shughuli za kiuchumi, ikieleza kuwa taarifa sahihi zina nafasi kubwa katika kuimarisha ufanisi wa sekta ya madini na shughuli zinazoizunguka.
Meneja Takwimu wa NBS Mkoa wa Geita, Khalid Msabaha, amesema takwimu rasmi zinawasaidia wadau kupata picha halisi ya mwenendo wa shughuli za kiuchumi na kufanya mipango inayozingatia taarifa zilizopimwa na kuthibitishwa.
Msabaha ametoa kauli hiyo wakati NBS ikishiriki katika Maonyesho ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita.
Amesema uwepo wa NBS katika maonyesho hayo unalenga kuongeza uelewa wa wadau kuhusu upatikanaji na matumizi sahihi ya takwimu, hasa katika sekta ya madini ambayo ina mchango mkubwa katika shughuli za uzalishaji na uchumi kwa ujumla.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na NBS, shughuli za uchimbaji wa madini zilichangia asilimia 10.3 ya Pato la Taifa mwaka 2025.
NBS pia imeeleza kuwa uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 6.1 katika robo ya kwanza ya mwaka 2026, ikilinganishwa na asilimia 5.9 mwaka 2025.
Msabaha amesema ongezeko hilo linaonyesha umuhimu wa kuwa na taarifa zinazopatikana kwa wakati ili kuwezesha wadau mbalimbali kufuatilia mabadiliko ya kiuchumi na kupanga shughuli zao.
Amesema katika maeneo kama Geita, ambako madini ni sehemu muhimu ya shughuli za kiuchumi, takwimu zinaweza kusaidia kuelewa kwa upana zaidi athari za sekta hiyo kwenye biashara, huduma, usafirishaji na ajira.
Ameongeza kuwa matumizi ya takwimu rasmi ni muhimu pia katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya taifa, ikiwemo Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050.
Ushiriki wa NBS katika maonyesho hayo umeelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi za kuwakutanisha wataalamu wa takwimu na wadau wa sekta ya madini, pamoja na kuhamasisha matumizi ya taarifa rasmi katika shughuli za uzalishaji, uwekezaji na maendeleo.

More Stories
Watendaji ,viongozi wapewa elimu ya udhibiti
Chawino kufanya uchaguzi mdogo
Barrick – Twiga yaunga mkono malengo ya Dira ya Taifa