Na Joyce Kasiki, Geita
MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) inaendelea kusimamia matumizi salama ya kemikali katika shughuli za uchimbaji wa madini, huku ikisisitiza umuhimu wa kupunguza matumizi ya zebaki na kuhamasisha matumizi ya teknolojia mbadala salama.
Hayo yamesemwa leo Septemba 30,2026 na Meneja wa Kanda ya Ziwa wa GCLA, John Wanjara Faustine, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonyesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, mkoani Geita.
Faustine amesema GCLA inasimamia sheria mbalimbali zinazohusu usimamizi na udhibiti wa kemikali nchini, ikiwemo usajili wa kemikali, wadau wanaozalisha au kuziingiza nchini, pamoja na maeneo zinakotumika.
Amesema mamlaka hiyo hufanya ukaguzi na kutoa elimu kwa watumiaji wa kemikali kuhusu matumizi sahihi na salama, hatua inayolenga kulinda afya za watumiaji, jamii na mazingira, hususan katika maeneo ya uchimbaji na uchenjuaji wa madini.
Kwa mujibu wa Faustine, GCLA pia ina maabara zilizoidhinishwa kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kimazingira, ubora wa bidhaa na kubaini uwepo wa madini mbalimbali, ikiwemo madini yanayoweza kuathiri mchakato wa uchenjuaji wa dhahabu.
Amesema huduma hizo huwawezesha wachimbaji na wadau wengine kupata taarifa sahihi za kimaabara na kuchukua tahadhari, ikiwa ni pamoja na kutumia njia mbadala kabla ya kuendelea na hatua za uchenjuaji.
Aidha, amesema Mkemia Mkuu wa Serikali ana jukumu la kusajili maabara za kemikali pamoja na maabara za kisayansi na jinai nchini ili kuhakikisha zinatoa huduma na majibu sahihi na ya kuaminika kwa wakati.
Katika eneo la tiba asili na tiba mbadala, Faustine amesema GCLA hushirikiana na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala chini ya Wizara ya Afya kupima usalama, ubora na viambata vya dawa zinazotokana na mimea.
Amesema mamlaka pia hutoa ushauri na elimu kwa wazalishaji wa dawa hizo kuhusu usindikaji bora na salama ili bidhaa zao zikidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.
Akizungumzia matumizi ya zebaki katika uchimbaji mdogo wa madini, Faustine amesema GCLA inaendelea kufuatilia matumizi ya kemikali hiyo katika maeneo ya uchimbaji, ikiwemo Geita, ili kuzuia madhara yake kuingia kwenye vyanzo vya maji na mazingira.
Amesema kwa mujibu wa Mkataba wa Minamata, matumizi ya zebaki yanalengwa kusitishwa ifikapo mwaka 2030, huku GCLA ikiendelea kutoa elimu kuhusu matumizi ya teknolojia na kemikali mbadala salama katika shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini.
Maonyesho hayo ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanaendelea mkoani Geita, yakilenga kuwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya madini na kuonesha teknolojia na huduma zinazoweza kuongeza usalama, ufanisi na tija katika shughuli za uchimbaji.

More Stories
Barrick – Twiga yaunga mkono malengo ya Dira ya Taifa
Umoja Afya ya NHIF yawavutia wengi Geita
Kurudi Shuleni baada ya Ujauzito,Safari yenye Miiba