Na Judith Ferdinand, TimesMajira,Mwanza
MBUNGE wa Jimbo la Nyamagana John Nzilanyingi, ameshauri Jiji la Mwanza pamoja na Majiji mengine na Manispaa kutumia mikopo na ubia na sekta binafsi kuharakisha uboreshaji wa miundombinu ya barabara.
Ambapo amesema kwa kasi ya sasa ya ujenzi, itachukua zaidi ya miaka 30 kukamilisha uwekaji wa lami kwenye mtandao wa barabara za jiji hilo.
Akizungumza Septemba 29,2026 na waandishi wa habari mkoani Mwanza, Nzilanyingi amesema,uharibifu wa miundombinu ya barabara ni miongoni mwa kero kubwa alizokutana nazo katika ziara zake za kusikiliza wananchi katika kata 16 kati ya 18 za Jimbo hilo.
Amesema Jiji la Mwanza lina mtandao wa barabara wenye urefu wa zaidi ya kilomita 1,025, huku kwa mwaka zikijengwa takribani km.3, pekee, hali ambayo inahitaji hatua za haraka kuongeza kasi ya uboreshaji wa miundombinu hiyo.
“Lengo la kwenda kwenye mikopo ni kuharakisha maendeleo, mfano Jiji letu la Mwanza linaweza kukopa sh.bilioni 50, 60 au 70 na kujenga kwa miaka mitano barabara ambazo kwa utaratibu wa sasa zingechukua zaidi ya miaka 20 kukamilika,”amesema Nzilanyingi.
Nzilanyingi amesema,Jiji la Mwanza lina makusanyo makubwa, huku makisio ya mapato kwa mwaka wa fedha 2026/27 yakifikia zaidi ya sh.bilioni 34, hivyo fedha hizo zinaweza kutumika kulipa mikopo hiyo kidogo kidogo kupitia mikataba na wakandarasi.
Katika hatua nyingine, Nzilanyingi amesema,Jimbo la Nyamagana bado linakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji, licha ya Serikali kutumia zaidi ya sh. bilioni 70 kujenga chanzo kipya cha maji cha Butimba, ambacho sasa kimekamilika na kinatoa huduma.
Amesema,baada ya mazungumzo yake na Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu changamoto hiyo, Serikali imetoa zaidi ya sh.bilioni 46 kwa ajili ya ujenzi wa matenki matano ya maji katika Jiji la Mwanza, ambapo matatu kati yake yatatumika kuhudumia wakazi wa jimbo hilo.
Hata hivyo amesema,ujenzi wa matenki hayo unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba mwaka huu, lakini akasisitiza kuwa kukamilika kwake pekee hakutamaliza tatizo la maji, kwa kuwa wananchi wanahitaji maji yafike kwenye mitaa yao.
“Nimezungumza na Waziri wa Maji Jumaa Aweso, na kumuomba aifikishe salamu zetu kwa Rais kwamba baada ya ujenzi wa matanki haya kukamilika, wananchi hawahitaji kuyaona maji kwenye matenki, wanahitaji wayaone maji kwenye mitaa yao,”amesema Nzilanyingi na kuongeza:
“Serikali imekubali kutoa fedha kwa ajili ya kujenga mtandao mpya wa usambazaji maji wenye urefu wa km.740 katika Jiji la Mwanza,kukamilika kwa matenki hayo pamoja na mtandao huo kutasaidia kumaliza tatizo la uhaba wa maji katika Jiji la Mwanza,”.
Sanjari na hayo amesema,amekuwa akifanya ziara katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Nyamagana kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi, pamoja na kutoa mrejesho wa shughuli anazozifanya akiwa Bungeni.

More Stories
Umoja Afya ya NHIF yawavutia wengi Geita
Kurudi Shuleni baada ya Ujauzito,Safari yenye Miiba
Dkt.Elisenguu:Acha sigara,pima moyo