Judith Ferdinand, TimesMajira Online,Mwanza
CHANGAMOTO ya baadhi ya wananchi kukosa huduma za matibabu kutokana na sababu mbalimbali imechochea Mbunge wa Jimbo la Nyamagana mkoani Mwanza, John Nzilanyingi, kuweka mikakati ya kusogeza huduma za afya za kibingwa karibu na wananchi wa Jiji la Mwanza.
Katika hatua hiyo, Mbunge huyo ameandaa kambi maalumu ya matibabu itakayowakutanisha madaktari bingwa na bobezi kutoka ndani na nje ya nchi, huku akieleza kuwa mpango huo ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa urahisi zaidi.
Akizungumza Septemba 29,2026 katika mkutano wake na waandishi wa habari mkoani Mwanza, Nzilanyingi amesema,kambi hiyo itafanyika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza kuanzia Oktoba 9 hadi 12, mwaka huu, na wananchi watapata huduma za uchunguzi, ushauri wa kibingwa na matibabu, ikiwemo operesheni ndogo na kubwa.
Nzilanyingi amesema,madaktari watakaoshiriki katika kambi hiyo watatoka katika taasisi mbalimbali za afya, zikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Mifupa na Ubongo (MOI), Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Hospitali ya Jeshi la Wananchi (MH), Hospitali ya Kanda ya Bugando, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure na Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana.
Amesema pia madaktari kutoka nchini India watashiriki katika kutoa huduma kwa wananchi wenye changamoto mbalimbali za kiafya ikiwemo magonjwa ya moyo.
“Madaktari hawa watakuja maalumu kwa ajili ya kutibu wananchi magonjwa mbalimbali, yakiwemo magonjwa ya moyo. Hivyo nawaomba wenye changamoto za kiafya katika sehemu mbalimbali kuweza kujisajili katika maeneo yao ili tuweze kupata idadi yao,”amesema Nzilanyingi.
Kwa mujibu wa Nzilanyingi, huduma zote katika kambi hiyo zitatolewa bure, huku akiwataka wananchi kujisajili mapema katika zahanati zilizo karibu nao pamoja na Kituo cha Afya Igoma, Kituo cha Afya Mkolani, Kituo cha Afya Bulale, Kituo cha Afya Fumagila na Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana.
Hata hivyo amesema,lengo la hatua hizo ni kusogeza huduma za afya za kibingwa kwa wananchi wa Jiji la Mwanza, akieleza kuwa katika kuwahudumia wananchi amekuwa akikumbana na changamoto ya baadhi yao kushindwa kupata matibabu.
Amesisitiza wananchi kutumia fursa hiyo kwa kujiandikisha mapema, akieleza kuwa hakutakuwa na muda wa nyongeza baada ya siku nne zilizopangwa kwa ajili ya kambi hiyo kumalizika.
Aidha, amesema mpango huo utaenda sambamba na hatua nyingine ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya bure kwa mwaka mzima, kupitia utoaji wa bima za afya 200 kwa wananchi wa jimbo hilo ambalo kila mtaa utapata bima moja kwa ajili ya mwananchi mmoja.

More Stories
Umoja Afya ya NHIF yawavutia wengi Geita
Kurudi Shuleni baada ya Ujauzito,Safari yenye Miiba
Dkt.Elisenguu:Acha sigara,pima moyo