Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka washiriki wa Maonesho ya Kimataifa ya Teknolojia na Akili Unde (Tech & AI International Expo 2026) kuyageuza majadiliano kuwa ushirikiano wenye matokeo kwa wananchi.
Katika maonesho hayo, Yas Tanzania imesema itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano na kuchochea huduma za kidigitali visiwani humo.
Akifungua maonesho hayo leo katika Hoteli ya Golden Tulip Zanzibar, Dkt. Mwinyi amesema teknolojia ina mchango mkubwa katika kuboresha huduma za afya, elimu na huduma za umma, pamoja na kufungua fursa za biashara na ajira.

“Maonesho haya yanatoa nafasi muhimu ya kubadilishana mawazo, kujenga ushirikiano, kuonesha ubunifu na kutafakari namna teknolojia inavyoweza kuchochea maendeleo yanayomfikia kila mmoja na kuijenga kesho yetu,” amesema Rais Mwinyi.
Amesema, manufaa ya teknolojia yanapaswa kuwafikia pia wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na wakazi wa maeneo ya pembezoni ambao hawajafikiwa na huduma.
Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Mudrick Ramadhan Soraga amesema vijana wanahitaji mazingira yatakayowawezesha kutumia ujuzi wa kidijitali kuanzisha biashara na kuhudumia wateja ndani na nje ya Zanzibar.
“Kijana wa Zanzibar anahitaji tu kuwa na wazo, kitendea kazi na huduma ya intaneti, kisha kujenga biashara inayohudumia wateja hapa nchini na hata nje ya mipaka yetu,” amesema Soraga.

Naye, Ofisa Mkuu wa Biashara wa Yas Tanzania, Norman Kiondo amesema kampuni hiyo itaendelea kuwekeza katika mtandao na kushirikiana na wadau kufikisha huduma za kidijitali kwa wananchi na biashara nyingi zaidi.
Amesema, kwa Zanzibar, Yas inashirikiana na ZICTIA kupanua huduma za intaneti ya (faiba) kuchochea huduma ya intaneti majumbani, taasisi na biashara Zanzibar ambapo imewekeza zaidi ya Sh bilioni 300.
Kwa mujibu wa Kiondo, Yas vilevile, imewekeza zaidi ya Sh. trilioni 1.2 katika mtandao wake nchini, na sasa ina zaidi ya minara 4,900 na zaidi ya kilomita 5,700 za miundombinu ya intaneti ya faiba.
Amesema, mawasiliano bora Zanzibar yatawezesha biashara za utalii kuwahudumia wageni, wajasiriamali kuwafikia wateja na taasisi za umma kutoa huduma kwa urahisi zaidi.

“Tutaendelea kuwekeza na kuboresha miundombinu yetu ya mawasiliano ili kuwa na mtandao imara hapa Zanzibar. Pia tutaendelea kushirikiana na Serikali na taasisi mbalimbali kusaidia biashara kutumia teknolojia na kuchochea ubunifu,” amesema Kiondo.

More Stories
Huduma za moyo Bugando zawanufaisha 1,200 kila mwezi
Serikali yasisitiza utekelezaji mpango ualbino
Wafugaji wasiosajiliwa Kibiti watakiwa kuondoka