September 29, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wafugaji wasiosajiliwa Kibiti watakiwa kuondoka

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Kibiti

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kibiti Mkoa wa Pwani, imewataka wafugaji wote wasiosajiliwa kuhakikisha hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Oktoba wawe wameondoka ili kuepuka migogoro baina yao na wakulima

Akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake, Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Kanali Mstaafu Joseph Kolombo amesema mifugo inayohama hama kwa ajili ya kusaka malisho ndiyo chanzo kikuu cha migogoro baina ya wafugaji na wakulima

Amesema, ili kumaliza migogoro hiyo wafugaji wote wanatakiwa kuhamia kwenye vitalu vyao na kuwataka kufuga mifugo wanayoweza kumudu kuilisha

“Acheni mara moja ufugaji usiozingatia taratibu fugeni mifugo mnayoweza kuimudu hususan kwenye kuilisha,” amesema Kanali Kolombo

Amesema, wilaya Ina vitalu zaidi ya 100 ambavyo vinatakiwa kuboreshwa na kuwa kwa kuwekewa maeneo ya majosho sambamba na maeneo ya malisho

Aidha, amewataka wafugaji kujiweka tayari kwa kuweka miundombinu inayostahili kwenye vitalu hivyo ikiwa ni pamoja na majosho kwa ajili ya kuogeshea mifugo

“Ili kumaliza migogoro wafugaji wote msiosajiliwa mnatakiwa kuhama mara moja na kwa wale waliosajiliwa hadi kufikia mwisho wa mwezi oktoba wawe wamekwenda kwenye vitalu vyao,” amesena Kanali Kolombo

Akizungumzia kuhusiana na tahadhali ya mvua za El Nino, amesema wilaya imejipanga na kuchukua tahadhari huku ikiwataka wananchi wanaoishi kwenye mazingira hatarishi kuhama kwenye maeneo hayo ili wabaki salama