September 29, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaombwa kuweka utaratibu kutatua migogoro wachimbaji wadogo


Na Joyce Kasiki, Geita

UKOSEFU wa uwazi kwenye mfumo wa umilikishaji wa maeneo ya uchimbaji unatajwa kuwa chanzo cha hasara kubwa kwa wachimbaji wadogo mkoani Geita, huku uwekezaji wao ukihatarishwa licha ya kufuata taratibu zote za Serikali.

Mfano wa hilo ni kwa Mchimbaji Mdogo, Tuguro Zakayo, ambaye amewekeza zaidi ya Shilingi milioni 230 kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi mitano, lakini sasa shughuli zimesimama baada ya kuondolewa eneo lake kwa madai kuwa linamilikiwa na mtu mwingine mwenye leseni.

Zakayo amesema licha ya kulipa mrabaha, kuwa na kumbukumbu kwenye vitabu na kufuata taratibu halali, wameondolewa ghafla na mtu aliyejitokeza akidai kuwa ana leseni ya eneo hilo hilo.

“Unavumbua eneo jipya na kuanza kuchimba, unatumia mtaji mkubwa kutafuta na kuchoronga. Ghafla anatokea mtu na leseni anakuambia uondoke. Huo ndio ukweli unaotuumiza,” amesema Zakayo.

Amesema tangu mwezi wa kwanza mwaka huu shughuli zimesimama na wanasubiri ufafanuzi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa, huku mitaji yao ikiwa imelala.

Kwa mujibu wake, changamoto mbili kubwa kwa wachimbaji wadogo ni mtaji na kutokuwa na uhakika wa maeneo wanayochimba, hali inayowafanya wengi kupata hasara baada ya uwekezaji mkubwa.

Ameiomba Serikali kuweka utaratibu wa kudumu na wa haraka wa kutatua migogoro ya leseni, ikiwemo kuweka mfumo unaoonyesha hadharani maeneo yaliyo na leseni na yale ambayo ni huru, ili mchimbaji mdogo ajue kabla ya kuwekeza.

Amesema utaratibu huo utalinda mitaji ya wachimbaji wadogo, kupunguza migogoro ya mara kwa mara na kuwapa uhakika wa kuwekeza kwa muda mrefu katika sekta ya madini.