October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Elimu afya ya uzazi nguzo imara kwa ustawi wa jamii

Na Judith Ferdinand TimesMajira Online, Mwanza

IMEELEZWA kuwa elimu ya afya ya uzazi ni nguzo imara kwa ustawi wa jamii kwa kuondokana na vitendo vya ukatili pamoja na mimba za mapema,hivyo kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kuhakikisha huduma rafiki za afya za uzazi kwa vijana zinapatikana sanjari na elimu sahihi huku wazazi kuwajibika kuwalea watoto wao.

Wito huo umetolewana Meneja Mipango,Mwanasheria wa Shirika la Wadada Solution on Gender Based Violence Anitha Samson,katika mkutano wa viongozi wa  kijamii na wadau mbalimbali juu ya uhamasishaji wa huduma rafiki ya afya ya uzazi kwa vijana na kupinga vitendo vya ukatili,uliondaliwa na shirika hilo uliofanyika jijini Mwanza.

Samson amesema,kuna wadau mbalimbali kama walimu,polisi wote wanashughulika na vijana hivyo wanatamani hao wote katika nafasi zao za kazi waweze kuhakikisha vijana wanapata huduma rafiki pale wanapohitaji kwani elimu ya afya ya uzazi kwa vijana ni ya msingi kwa sababu  vijana wengi wanapata changamoto ya kupata taarifa ambayo siyo sahihi  kwenye jamii.

Amesema jamii nyingi hazifanyi kazi na vijana kwa namna moja ama nyingine wanaona elimu ya  afya ya uzazi kuwafundisha inakuwa  ngumu kuzungumza na ina maneno magumu hii ni kutokana na kugubikwa na mila na desturi ambazo siyo rafiki  hivyo wanajikuta wanashindwa kuelewa ni sehemu gani wapate elimu hiyo.

“Elimu ya afya ya uzazi kwa vijana ina umuhimu sana kwa kuwaepusha vijana na mimba za utotoni,kuingia katika mahusiano wakiwa katika umri mdogo ambao unaathiri  via vya uzazi na masomo yaokwa ujumla,jamii kwa ujumla kuungana kwa pamoja kuhakikisha kijana anapata taarifa sahihi kuhusiana na makuzi,mabadiliko ya mwili na kuwakinga na mimba na ndoa za utotoni,lengo ni kuhakikisha tunaishi katika jamii salama bila ukatili na mazingira salama hususani watoto wa like ambao ndio kundi kubwa linaloathirika,”amesema Samson.





Baadhi ya washiriki wa mkutano wa viongozi wa kijamii na wadau mbalimbali juu ya uhamasishaji wa huduma rafiki ya afya ya uzazi kwa vijana na kupinga vitendo vya ukatili uliondaliwa na shirika la Wadada Solution on Gender based Violence uliofanyika jijini Mwanza.picha na Judith Ferdinand

Akizungumzia suala la wazazi kuwalea watoto wao Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kwimba Revina Theognance, amesema wazazi wasichoke kuwalea watoto kwani kumekuwa na tabia ya kuwapeleka watoto wadogo shule za bweni na wasiwapeleke kwa bibi bali wawalee wenyewe ili kuwaepusha na vitendo vya ukatili huku walimu nao wasichoke kuwafundisha kwani muda mwingi ndio wanashindwa nao.

Kwa upande wake Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto Jiji la Mwanza,Bertha Yohana amesema idadi kubwa ya vijana walio katika balehe hujihusisha na vitendo vya ngono isiyo salama na kutokana na takwimu za watu na hali ya afya ya mwaka 2010 ( TDHS 2010) inaonyesha vijana wanakabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwemo ya kujihusisha na vitendo vya kujamiiana.

Amesema takwimu hizo  zinaonesha kuwa wasichana wengi huanza kujihusisha na ngono wakiwa na umri wa miaka 18,ambao ni  asilimia 59 wakati wavulana huanza wakiwa na miaka 20 amabao ni asilimia 45 pia zinaeleza kuwa wasichana kati ya umri wa miaka 15-24,asilimia 13 wameshajamiiana kwenye umri wa miaka 15; ukilinganisha na asilimia 7 kwa wavulana.

Mimba katika umri mdogo ni miongoni mwa matatizo makubwa ya afya ya uzazi kwa vijana hapa nchini,kutokana na takwimu hizo, vifo vya watoto waliozaliwa na wamama walio chini ya umri wa miaka 20 ni vifo  111 kwa vizazi 1,000,ukilinganisha na wale wa umri wa miaka 30 -39 ambavyo ni vifo 93 kwa vizazi 1,000 na  wasichana wengi baada ya kuzaa hupoteza nafasi ya kuendelea na masomo na shughuli nyingine za kiuchumi na hivyo kutumbukia katika umasikin mkali.

Pia amesema,ili kupunguza na hatimaye kuwaondolea vijana matatizo hayo Kila kiongozi wa serikali, dini na mashirika yasiyo ya kiserikali katika ngazi zote wanapaswa,kutetea sera za kuboresha huduma za afya ya uzazi kwa vijana,kutetea na kuokoa maisha ya vijana kwa kuboresha afya y uzazi kwa kundi hilo,kuweka matatizo ya vijana kuwa ni agenda muhimu katika shughuli zao kila siku.

Naye Mkuu wa  Polisi Wilaya ya Ilemela (OCD) Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Elisante Ulomi, amesema kwa namna moja vitendo hivyo vimekuwa vimisitisha ndoto za wanafunzi,kumekuwa na shida kubwa ya mimba shuleni hivyo kumekuwa na mfumo ambao unakwamisha ufuatiliaji kutokana na wazazi wa binti kuanza kujadiliana na mlengwa hivyo kesi ikifika mahakamani mashahidi hawafiki kutoa ushahidi.

Hata hivyo Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Polisi Wilaya ya Ilemela Inspector Hilda Maleko,ni kweli wanafunzi wanapata mimba lakini wao kama Polisi katika kufanya jitihada za kukomboa kundi hilo wamekuwa wakipita shuleni kutoa elimu kuhusu ukatili na mimba za utotoni pamoja na kuwaeleza madhara ya kujihusisha na mapenzi katika umri mdogo na umuhimu wa elimu ya afya ya uzazi.