September 28, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mama Zainabu:Mazoezi kinga ya maradhi

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

MKE wa Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Taifa, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mama Zainab Kombo Shaib, amewahimiza akina mama kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi ili kulinda afya zao na kuepuka maradhi mbalimbali.

Mama Zainab ametoa wito huo alipokuwa akisalimiana na kujumuika nao katika mazoezi,
wanachama wa kikundi cha mazoezi cha Wazalendo Kinamama Fitness Group, kilichopo katika kijiji cha Wingwi Jambo-nia, Jimbo la Wingwi, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Amesema mazoezi kama sehemu ya maisha ya kila siku, ni njia bora ya kujikinga na maradhi, hususan yale yasiyo ya kuambukiza.

“Mazoezi ya mwili ni muhimu sana kwetu, kwani katika umri tuliofikia tuko kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata maradhi nyemelezi. Mwili ni kama mashine; isipotumika huzeeka, huchakaa na kuharibika. Ndivyo ulivyo pia mwili wa binadamu,” alisisitiza Mama Zainab.

Aidha, ameeleza kuwa maradhi yasiyo ya kuambukiza—kama vile kisukari na shinikizo la damu—kwa kiasi kikubwa huchangiwa na ulaji wa vyakula visivyo salama au vya kusindikwa. Hivyo, amewasisitiza wananchi kuzingatia ulaji wa vyakula vya asili na kufanya mazoezi, akibainisha kuwa “mazoezi ni dawa.”

Ameongeza kuwa juhudi hizo za akina mama watu wazima zitawasaidia kuwa imara kimwili na kuijenga jamii yenye afya tele.

“Jambo hili lisiishie kwetu watu wazima tu, bali tuwashawishi na kuwahimiza wababa pamoja na watoto wetu, kwani mazoezi ni kinga—na kinga ni bora kuliko tiba,” alisema.

Akisoma risala kwa niaba ya kikundi hicho, Bi. Maryam Said, alisema kikundi chao kilichoanzishwa mnamo Juni 27, 2026, hivi sasa kina jumla ya wanachama 80.

Hata hivyo, alibainisha kuwa kinakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo ukosefu wa vifaa vya mazoezi kama vile sare, viatu pamoja na spika kwa ajili ya kuongeza hamasa wakati wa mazoezi.

Katika hafla hiyo, Mama Zainab alikabidhiwa rasmi ulezi wa kikundi hicho-wadhifa ambao aliupokea kwa mikono miwili na kuahidi kushirikiana nao bega kwa bega, ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kupata mahitaji yao ili kuboresha ufanisi wa mazoezi yao.

Akitoa neno la shukrani, Mwenyekiti wa kikundi hicho, Maryam Hamad Hamad, pamoja na Kocha wao wa Mazoezi,Kombo Hamad Othman, walieleza kuwa wanaendelea na jitihada za kuandikisha wanachama zaidi katika kikundi hicho ambacho kimekuwa chachu kubwa ya mabadiliko jimboni humo.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama cha ACT-Wazalendo ngazi ya mkoa (Micheweni) na jimbo, akiwemo Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Wingwi, Mhe. Juma Kombo Hamad, na Katibu wa Ngome ya Wanawake Mkoa, Bi. Batuli Mussa Sharif.