September 26, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

EWURA yatoa elimu Nishati, Maji maonyesho Geita


Na Joyce Kasiki, Geita


MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetumia Maonyesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika Viwanja vya Samia Suluhu Hassan mkoani Geita kutoa elimu kwa wananchi na wadau kuhusu huduma za nishati na maji inazozidhibiti.


Akizungumza katika maonyesho hayo, Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, Nyirabu Musira , amesema ushiriki wa mamlaka hiyo unalenga kuwaelimisha wananchi kuhusu huduma za nishati na maji, pamoja na fursa na taratibu mbalimbali zinazohusiana na sekta hizo.


Amesema Kanda ya Ziwa ya EWURA inahusisha mikoa ya Mwanza, Geita, Simiyu, Mara na Kagera, ikiwa na makao makuu jijini Mwanza.


Bushira amesema EWURA pia inaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuongeza matumizi ya nishati hiyo.


Katika hatua nyingine, amesema EWURA imepunguza masharti na gharama za uwekezaji katika vituo vya mafuta vijijini kwa zaidi ya asilimia 90, hatua inayolenga kuchochea uwekezaji katika maeneo hayo na kupunguza uuzaji holela wa mafuta.


Ameeleza kuwa ada ya maombi ya leseni ya kituo cha mafuta mijini ni Shilingi 500,000, wakati vijijini ni Shilingi 50,000. Aidha, ada ya leseni ya miaka mitano ni Shilingi milioni moja mijini, huku vijijini ikiwa Shilingi 100,000.


Mbali na masuala ya nishati, EWURA imeendelea kuhamasisha wananchi kuhusu uvunaji wa maji ya mvua kama njia mojawapo ya kuongeza upatikanaji wa maji kwa matumizi mbalimbali.


Kwa upande wake, Afisa Mawasiliano na Hifadhi Mazingira wa EWURA, Tobieth Makafu, amewaalika wananchi wa Geita na Kanda ya Ziwa kutembelea banda la EWURA katika Viwanja vya Samia Suluhu Hassan ili kupata elimu kuhusu huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo.


Makafu pia amewataka mafundi umeme wasio na leseni kufika katika banda hilo kwa ajili ya kupata elimu na kufahamu utaratibu wa kupata leseni rasmi ya kufanya shughuli za ufundi umeme.


Aidha, amesema EWURA inapokea kero na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu huduma za mamlaka za maji pamoja na TANESCO, hususan malalamiko ambayo hayajapatiwa utatuzi.


Amesema wananchi wanapata fursa ya kuwasilisha changamoto zao kupitia banda la EWURA ili zipokelewe na kufanyiwa kazi kwa mujibu wa taratibu.