WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imefanya marekebisho ya ratiba ya upimaji na mitihani ya Taifa kwa mwaka 2026, kwa lengo la kuzuia athari zinazoweza kujitokeza kutokana na uwezekano wa mvua kubwa za El Nino zinazotarajiwa katika baadhi ya maeneo nchini.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam, Septemba 25, 2026, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, amesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya Serikali kufuatilia kwa karibu taarifa za hali ya hewa na kutathmini athari zinazoweza kujitokeza katika uendeshaji wa upimaji na mitihani ya Taifa.
Amesema kwa mujibu wa utabiri rasmi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, kuna uwezekano wa kutokea kwa El Nino yenye nguvu, huku mvua zikitarajiwa kuanza katika baadhi ya maeneo mwezi Oktoba 2026 na kuwa nyingi zaidi mwezi Novemba 2026, hali ambayo inaweza kuathiri usafiri na kufikika kwa baadhi ya vituo vya mitihani.
Ameeleza kuwa kwa kuzingatia jiografia ya nchi na uwezekano wa baadhi ya maeneo kukumbwa na mafuriko, changamoto za usafiri na athari nyingine zinazoweza kusababishwa na hali ya hewa, Wizara kwa kushirikiana na Baraza la Mitihani la Tanzania imefanya marekebisho ya ratiba ya upimaji na mitihani ya Taifa.
Kwa mujibu wa ratiba iliyorekebishwa, Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Pili Ngazi ya Shule utafanyika Oktoba 7 hadi 8, 2026, wakati Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne utafanyika Oktoba 5 hadi 6, 2026.
Aidha, Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili utafanyika Oktoba 12 hadi 23, 2026, huku Mitihani ya Kidato cha Nne ikifanyika kuanzia Oktoba 19 hadi Novemba 6, 2026.
Amesema marekebisho hayo yanalenga kuhakikisha usalama wa wanafunzi, walimu, wasimamizi, maafisa na wadau wengine wanaohusika na uendeshaji wa mitihani, pamoja na kulinda mitihani, vifaa na nyaraka muhimu.
Ameongeza kuwa iwapo ratiba ya awali ingeendelea na mvua kubwa zikajitokeza mwezi Novemba 2026, changamoto zingeweza kujitokeza katika usafirishaji na ufikishaji wa mitihani, vifaa na nyaraka muhimu katika vituo, huku wanafunzi na wasimamizi wakikabiliwa na ugumu wa kufika kwa wakati kutokana na mafuriko na uharibifu wa barabara.
Wizara imeendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa hali ya hewa na kuchukua hatua stahiki kwa kushirikiana na mamlaka na taasisi husika, ili kuhakikisha upimaji na mitihani ya Taifa inafanyika kwa utaratibu unaofaa, huku usalama wa wanafunzi, walimu, wasimamizi na wadau wengine ukipewa kipaumbele.

More Stories
Mkenda aungana na wadau kuimarisha elimu Duniani
Serikali yaandaa vijana kwa uchumi kidigitali
Karatu: Visima vya Umwagiliaji Kumkomboa Mkulima