Na Mwandishi Wetu, TimesMajira
WANAFUNZI wa Shule ya Msingi Buigiri mkoani Dodoma, wakiwemo wenye changamoto ya uoni na ualbino, wamepata msaada wa vifaa na mahitaji mbalimbali kutoka Yas Tanzania kwa ajili ya kusaidia mazingira yao ya shule.
Msaada huo umejumuisha mitungi ya gesi, mchele, maharage, mafuta ya kupikia, sabuni za kufulia na mafuta ya kupaka pamoja na kofia maalum kwa watoto wenye ualbino. Yas pia iligharamia mahafali ya wanafunzi wa Darasa la Saba yaliyofanyika shuleni hapo.
Shule ya Msingi Buigiri ilianzishwa mwaka 1950 na ni miongoni mwa shule zenye historia kubwa nchini katika kutoa elimu kwa watoto wenye changamoto ya uoni na ualbino.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Mkuu wa Yas – Kanda ya Kati, Said Idd, amesema kampuni hiyo iliamua kuisaidia shule hiyo baada ya kuona umuhimu wa kuwawezesha wanafunzi kupata baadhi ya mahitaji muhimu wanayotumia kila siku.
“Mtoto anahitaji zaidi ya darasa ili afanye vizuri katika masomo. Anahitaji chakula na mahitaji mengine ya msingi yatakayomwezesha kusoma kwa utulivu. Tumekuja Buigiri kuchangia katika mahitaji hayo na kuwaunga mkono watoto hawa katika safari yao ya elimu,” amesema Idd.
Amesema, uwepo wa Yas katika jamii hauishii kwenye huduma za mawasiliano pekee, bali kampuni hiyo imekuwa ikishiriki katika shughuli za elimu, afya na maeneo mengine yenye mahitaji katika jamii.
“Tunapozungumzia Mtandao wa Viwango, hatuzungumzii ubora wa mawasiliano pekee. Tunataka uwepo wetu uonekane pia katika jamii tunayoihudumia,” amesema Idd.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Wadau wa Elimu Dodoma, Jesca Makaula, ameipongeza Yas kwa msaada huo, akisema mahitaji yaliyotolewa yatasaidia shule pamoja na wanafunzi katika shughuli zao za kila siku.
“Watoto hawa wana ndoto kama watoto wengine. Msaada kama huu unawasaidia kupata baadhi ya mahitaji muhimu na pia unawapa moyo wa kuendelea na masomo yao. Tunaomba wadau wengine waendelee kujitokeza na kushirikiana na shule zetu,” amesema Makaula.
Yas pia iliungana na wanafunzi wa Darasa la Saba katika mahafali yao na kuwahimiza kuendelea na elimu, kujiamini na kutokata tamaa katika kufikia malengo yao.

More Stories
NMB yaingia 10 Bora Duniani
Waziri Salome ashiriki ufunguzi Gastech 2026 Bangkok
Kijana apigwa risasi tuhuma za uhalifu benki