September 1, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaanza mchakato kutambua Madaktari wenye ubobezi

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma

SERIKALI  imesema imepokea mapendekezo ya Muundo wa Utumishi kwa wataalamu wa kada ya afya wenye elimu ya ngazi ya ubobezi, huku taratibu za uchambuzi wa kina na kupata idhini zikiendelea.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Qwaray, wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbulu Vijijini, Dkt. Emmanuel Qambaji Nuwas, bungeni jijini Dodoma.

Dkt. Qambaji alitaka kujua mpango wa Serikali wa kutambua kwenye Muundo wa Utumishi wa Umma wataalamu wa kada ya afya wenye elimu ya ngazi ya ubobezi.

Akijibu, Qwaray amesema miundo ya maendeleo ya utumishi huandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya kiutumishi, majukumu ya kada husika, pamoja na viwango vya elimu na sifa za kitaaluma vinavyotolewa na taasisi za elimu zilizoidhinishwa.

Amesema Wizara inayosimamia Utumishi tayari imepokea mapendekezo ya Muundo wa Utumishi kwa wataalamu wa kada ya afya wenye elimu ya ngazi ya ubobezi.

“Tarati­bu kwa ajili ya uchambuzi wa kina na kupata idhini zinaendelea,” alisema Kwaray.
Hatua hiyo inaashiria kuwa Serikali ipo katika mchakato wa kuangalia namna ya kutambua wataalamu hao ndani ya Muundo wa Utumishi wa Umma, kwa kuzingatia mahitaji ya kiutumishi na sifa zao za kitaaluma.”amesema