September 1, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuboresha hadhi ,maslahi ya madereva

Na Joyce Kasiki, Timesmajira online,Dodoma

SERIJALI  imesema inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha taaluma na kazi ya udereva inapata staha, hadhi na heshima sawa na kada nyingine katika utumishi wa umma.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Qwaray, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mlalo, Rashid Abdallah Shangazi, Bungeni.

Shangazi alitaka kujua mkakati wa Serikali wa kuhakikisha taaluma na kazi ya udereva inakuwa na staha, hadhi na heshima sawa na kada nyingine.

Akijibu swali hilo, Qwaray amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuboresha Muundo wa Maendeleo ya Utumishi wa Kada ya Udereva.

Amesema Serikali pia inaendelea kuboresha mafunzo ya kitaaluma pamoja na viwango vya elimu kwa kada hiyo, hatua inayolenga kuongeza weledi na uwezo wa watendaji katika kutekeleza majukumu yao.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, Serikali vilevile imeendelea kuimarisha motisha na maslahi ya kada ya udereva ili kukidhi na kumudu mazingira ya utendaji kazi.

Hatua hizo, amesema, ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha kada ya udereva inathaminiwa na kupewa hadhi inayostahili katika utumishi wa umma.