September 1, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Fursa mafunzo ufundi kwa wanawake zaongezwa

Na Mwandishi Wetu , Dodoma

SERIKALI imeeleza kuwa inaendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya kuwapatia wanawake mafunzo ya ufundi stadi kwa lengo la kuwawezesha kuibua fursa za kibiashara, kujiajiri na kuongeza kipato.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Fatma  Rembo, kuhusu mpango wa Serikali wa kuwapatia wanawake mafunzo ya ufundi stadi ili kuwawezesha kuibua fursa za kibiashara.

Naibu Waziri Mahundi amesema Serikali, kupitia mipango mbalimbali ya kisekta, inaendelea kutoa fursa za mafunzo ya ufundi stadi kwa wanawake ili kuwawezesha kupata ujuzi wa kuwaongezea uwezo katika shughuli za kiuchumi.

Amesema miongoni mwa hatua zinazotekelezwa ni Mradi wa Uwezeshaji kupitia Ujuzi unaolenga wasichana wenye umri wa miaka 18 hadi 35. Hadi Juni 2026, jumla ya wasichana 1,051 walikuwa wamefikiwa na mradi huo.

Aidha, amesema kupitia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Serikali inaendelea kutoa mafunzo ya vitendo kwa wanawake katika fani mbalimbali, zikiwemo ushonaji, utengenezaji wa bidhaa na matumizi ya teknolojia.

Amesema pia Serikali inaendelea kutekeleza Programu ya Utambuzi na Urasimishaji Ujuzi, inayolenga kutambua na kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu.

Hadi Juni 2026, jumla ya vijana 14,400, sawa na asilimia 18 ya lengo, kutoka mikoa 11 walikuwa wamesajiliwa katika programu hiyo, inayolenga kuwafikia vijana 80,000 ifikapo Juni 2027.

Sambamba na hayo, amesema Vyuo vya Maendeleo ya Jamii pamoja na Vyuo vya Ufundi vya Mabughai na Misungwi vinaendelea kutoa mafunzo katika fani za uhandisi wa ujenzi na maendeleo ya jamii.

Katika mwaka wa masomo 2025/26, jumla ya wanachuo 1,087 walihitimu mafunzo katika vyuo hivyo, ambapo wasichana walikuwa 496, sawa na asilimia 46.