Na Joyce Kasiki, Tanga
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian, amezindua rasmi Programu ya InnoIP Tanzania, inayolenga kuwawezesha wabunifu, watafiti, kampuni changa na wajasiriamali kulinda, kusimamia na kubiasharisha bunifu zao ili kuongeza thamani ya kiuchumi na kijamii.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo Agosti 22,2026 Balozi Batilda amesema programu hiyo ni hatua muhimu katika kujenga mazingira ambayo mawazo na ubunifu wa Watanzania yanaweza kubadilishwa kuwa bidhaa, huduma na biashara zenye ushindani.
Amesema Programu ya InnoIP inatekelezwa kwa ushirikiano wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), kupitia Dar Teknohama Business Incubator (DTBi) na Buni Innovation Hub, pamoja na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).
Kwa mujibu wa Balozi Batilda, programu hiyo haitajikita katika semina za uhamasishaji pekee, bali itatoa warsha za vitendo, mafunzo ya kila mwezi kwa njia ya mtandao, tathmini za ubunifu, kliniki za miliki bunifu, ushauri elekezi na msaada wa kuwasilisha maombi ya ulinzi wa miliki bunifu.
Amesema programu hiyo pia itawawezesha wabunifu kuelewa aina ya ulinzi inayofaa kwa bunifu zao, kuboresha nyaraka na kuunganisha miliki bunifu zilizolindwa na fursa za utoaji wa leseni, uwekezaji, ushirikiano wa kibiashara na masoko.
“Programu ya InnoIP haitakomea katika semina za kujenga uelewa pekee. Itatoa warsha za vitendo, mafunzo ya kila mwezi kwa njia ya mtandao, tathmini binafsi za ubunifu, kliniki za ubunifu na miliki bunifu pamoja na ushauri elekezi,” amesema.
Balozi Batilda amesema katika mwaka wa kwanza programu hiyo inalenga kuwafikia washiriki wasiopungua 5,000 na kufanya tathmini za kina kwa wabunifu 120, akizitaka taasisi zinazotekeleza programu hiyo kuhakikisha matokeo yanaonekana na kupimika.
Aidha, amesema teknolojia ni nyenzo muhimu katika uendeshaji na ukuaji wa biashara, hususan kupitia majukwaa ya kidijitali, biashara mtandao, huduma za kifedha za kidijitali, akili unde na mifumo ya kidijitali ya kusimamia biashara.
Amesema wanawake wajasiriamali wanapaswa kushiriki kikamilifu katika mageuzi ya kidijitali, huku akitaja Programu ya Fursa Women inayolenga kuwajengea uwezo wanawake kuhusu matumizi sahihi, salama na yenye tija ya teknolojia katika biashara.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu na mwakilishi wa Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Loy Mhando, amesema Programu ya InnoIP imeanzishwa kutokana na changamoto zinazowakabili wabunifu nchini, wakiwamo wale wanaoweka wazi mawazo yao mapema, kushindwa kuweka kumbukumbu sahihi za uendelezaji wa vumbuzi na kuanza kushughulikia masuala ya miliki bunifu baada ya bidhaa kuingia sokoni.
Amesema hali hiyo inaweza kusababisha mbunifu kupoteza fursa ya kupata ulinzi unaofaa, kampuni changa kukumbwa na migogoro ya umiliki na wawekezaji kusita kuwekeza kutokana na kutokuwepo kwa uthibitisho wa umiliki wa rasilimali za kiubunifu.
“Programu ya InnoIP Tanzania imeanzishwa ili kukabiliana na changamoto hizi kwa kuwasaidia wabunifu kufanya maamuzi sahihi kwa wakati unaofaa,” amesema.
Mhando amesema programu hiyo si kwamba inalenga kila ubunifu upewe hataza au aina nyingine ya ulinzi, bali inamsaidia mbunifu kutambua mchanganyiko unaofaa wa mbinu za ulinzi na usimamizi wa miliki bunifu, zikiwamo hataza, maumbo bunifu, alama za biashara, hakimiliki, siri za biashara, mikataba ya usiri na mikataba ya leseni.
Amesema walengwa wa programu hiyo ni kampuni changa, wabunifu walio katika hatua za awali, watafiti, wanafunzi wa vyuo vikuu, biashara ndogo na za kati, biashara zinazoongozwa na wanawake na vijana, vituo vya ubunifu, vituo vya uatamiaji wa biashara na taasisi za utafiti.
Ameeleza kuwa safari ya mbunifu kupitia InnoIP itahusisha hatua saba, ambazo ni utambuzi na uhamasishaji, mafunzo, uchambuzi wa mahitaji, maandalizi, ulinzi, ubiasharishaji na ufuatiliaji.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, amesema uzinduzi wa InnoIP Tanzania ni matokeo ya ushirikiano kati ya COSTECH na BRELA katika kujenga mfumo unaomwezesha mbunifu kutoka hatua ya wazo hadi ulinzi wa miliki bunifu, uwekezaji na soko.
Amesema kupitia Buni Innovation Hub, COSTECH huwasaidia wabunifu walio katika hatua za awali kukuza suluhisho zao, kuthibitisha uhalisia na uhitaji wa mawazo yao na kujenga biashara zinazoweza kukua na kudumu.
Amesema DTBi nayo inalenga kusaidia kampuni changa na teknolojia zilizo tayari kuingia katika hatua za uatamizi, ubiasharishaji, uwekezaji na masoko, huku BRELA ikitoa utaalamu unaohitajika katika masuala ya miliki bunifu na ulinzi wa bunifu hizo.
Dkt. Nungu amesema kaulimbiu ya programu hiyo ni “Kutoka Wazo hadi Thamani: Kulinda Ubunifu wa Watanzania, Kujenga Biashara na Ajira.”
Amesema Tanzania ina vijana, watafiti, wabunifu na wajasiriamali wenye mawazo na teknolojia zenye uwezo wa kutatua changamoto za jamii na kujenga biashara, lakini changamoto kubwa ni kuhakikisha mawazo hayo yanalindwa, yanaendelezwa na kufika sokoni.
“Miliki bunifu si suala la kisheria pekee; ni rasilimali ya kiuchumi,” amesema Dkt. Nungu.
Amesema katika mwaka wa kwanza, COSTECH na wadau wake wanalenga kuwafikia watu wasiopungua 5,000, kufanya tathmini ya mahitaji ya miliki bunifu kwa wabunifu wasiopungua 120 na kusaidia hatua muhimu za ulinzi wa miliki bunifu zisizopungua 20.
Dkt. Nungu amesema mafanikio ya programu hiyo hayatapimwa kwa idadi ya watu waliohudhuria mafunzo pekee, bali pia kwa kuongezeka kwa ubunifu unaolindwa, teknolojia zinazoingia sokoni, biashara zinazokua, uwekezaji unaovutwa na ajira zinazozalishwa.
Sambamba na uzinduzi wa InnoIP Tanzania, Dkt. Nungu amesema shughuli hizo zimefuatiwa na Programu ya Fursa Women, inayotekelezwa na COSTECH kwa ushirikiano na Airtel Tanzania, kwa lengo la kuwajengea uwezo wanawake wafanyabiashara na wajasiriamali kutumia teknolojia kuanzisha, kuendesha na kupanua biashara zao.
Amesema ushirikiano huo unaonesha umuhimu wa sekta ya umma na binafsi kufanya kazi kwa pamoja katika kujenga jamii yenye ujuzi wa kidijitali na kuhakikisha wanawake hawabaki nyuma katika mabadiliko ya teknolojia.

More Stories
Rais Samia aagiza wakuu wa Mikoa kujiandaa na udhibiti wa Athari za El Nino
Ndejembi:Tanzania sasa inaziada ya Umeme Megawati 2375
Rais Samia azindua kituo cha JNHPP