August 22, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ubunifu wawekwa mbele katika mpango mpya wa Taifa



Na Joyce Kasiki, Tanga


SERIKALI imeeleza kuwa inaendelea kuweka mazingira yatakayowezesha elimu, utafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu kuwa kichocheo kikuu cha maendeleo ya Taifa, huku ikisisitiza matumizi ya maarifa kutatua changamoto zinazolikabili Taifa.


Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Ladislaus Mnyone, alisema hayo wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Kitaifa la Elimu, Utafiti, Ujuzi na Ubunifu lililofanyika Tanga huku akisema jukwaa hilo ni sehemu ya juhudi za kuunganisha elimu, utafiti, ujuzi na ubunifu ili kujenga msingi wa maendeleo endelevu na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.


Amesema Serikali imeandaa Mpango Mkuu wa Taifa wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (National STI Master Plan), unaoweka vipaumbele na mwelekeo wa kimkakati katika kujenga uwezo wa nchi kupitia sayansi, teknolojia na ubunifu.


Kwa mujibu wa Profesa Mnyone, hatua nyingine inayochukuliwa ni kuwashirikisha Watanzania wanaoishi nje ya nchi kwa kutumia maarifa na uzoefu wao katika kuendeleza elimu, tafiti, teknolojia na ubunifu.


Amesema mkakati maalumu wa kuwashirikisha diaspora katika sekta hizo tayari unaanza kutekelezwa, hatua inayolenga kuongeza mchango wa wataalamu hao katika maendeleo ya Taifa.


Pia, wizara imefikia hatua ya kukamilisha rasimu ya National Technology Roadmap, ambayo itaainisha mahitaji na maeneo muhimu ya kiteknolojia kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.


Jukwaa hilo lenye kaulimbiu “Kujenga Msingi Imara Unaotegemea Ujuzi kwa Ajili ya Elimu Bora, Ubunifu na Maendeleo Endelevu,” ambalo limewakutanisha wadau mbalimbali kutoka katika sekta za elimu, utafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu.


Mwenyekiti wa jukwaa hilo na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Profesa Raphael Chibunda, amesema mafanikio katika sayansi na teknolojia yanahitaji ushirikiano mpana kati ya Serikali, vyuo, watafiti, wabunifu na sekta binafsi.


Amesema matumizi sahihi ya teknolojia na matokeo ya tafiti yanapaswa kuelekezwa katika kuongeza tija na kutengeneza suluhisho zinazogusa mahitaji halisi ya jamii, hasa kwa vijana.


Ameongeza kuwa ushirikiano huo unaweza kusaidia kubaini changamoto mapema, kukuza ubunifu na kuwezesha wataalamu kupata fursa ya kugeuza maarifa yao kuwa suluhisho zenye manufaa kwa wananchi.